Wanaongezeka; Thomas Ulimwengu, mmoja wa Watanzania wanaocheza nje, idadi sasa itaongezeka |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania, Gossage Mtumwa ili aweze kucheza soka nchini Yemen.
Mtumwa ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Soka Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo.
TFF inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu nchini Yemen.
Wakati huo huo: Kamisaa Alfred Kishongole Rwiza ameteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuhudhuria semina ya makamishna itakayofanyika kuanzia Julai 6-7 mwaka huu katika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri.
Semina hiyo inashirikisha baadhi ya makamishna wa CAF walioko kwenye orodha ya makamishna ya shirikisho hilo kwa mwaka 2012-2014.
Rwiza ni mmoja wa makamishna wa CAF kutoka Tanzania, na mechi ya mwisho kusimamia ilikuwa ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Mei mwaka huu nchini Msumbiji.
CAF tayari imeshamtumia tiketi Rwiza, na anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kwenda Cairo kwa ndege ya EgyptAir.