• HABARI MPYA

        Saturday, June 08, 2013

        KIM POULSEN AWAANZISHA PAMOJA NGASSA, SAMATTA NA ULIMWENGU DHIDI YA MOROCCO LEO

        Mashine tatu; Kutoka kulia Ulimwengu, Samatta na Ngassa, Waarabu watatoka?
        Na Mahmoud Zubeiry, Marakech, IMEWEKWA JUNI 8, 2013 SAA 5:20 ASUBUHI
        KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars atawaanzisha pamoja washambuliaji wawili wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu katika mchezo wa usiku wa leo dhidi ya wenyeji, Morocco, Simba wa Atlasi Uwanja wa Marakech mjini hapa.
        Kama alivyosema jana, Mdenmark huyo ameamua kutumia mfumo wa kushambulia moja kwa moja katika mchezo huo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, akitumia mfumo wa 4-3-3 ambao amekuwa akiutumia kipindi cha pili katika mechi za zilizopita.
        Katika mechi zake tano zilizopita nyumbani ambazo Stars ilishinda, Kim amekuwa akianza na mfumo wa 4-4-2 na baadaye kipindi cha pili anabadilisha na kuhamia kwenye 4-3-3 kuongeza kasi ya mashambulizi na mara nyingi huo ndiyo umekuwa wakati ambao mabao ya Stars yanapatikana.
        Katika mchezo wa leo ambao ni muhimu Stars kushinda, Kim amebadilisha mipango yake ili kutafuta ushindi wa mapema. 
        Kocha Poulsen kushoto akijadiliana na wasaidizi wake, Sulvester Marsh Jacob Michelsen jana Uwanja wa Marakech 
        Mazoezi ya ndondi; Wachezaji wa Stars wakifanya mazoezi ya ndondi jana, Zahor Pazi kulia na Erasto Nyoni kushoto
        Vijana wako tayari; Pamoja na rabsha zote, wachezaji wa Stars wanaonekana kuwa imara

        Juma Kaseja leo atalindwa na Shomary Kapombe kulia, Erasto Nyoni kushoto na Kevin Yondan na Aggrey Morris katikati wakati viungo watakuwa watatu Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Amri Kiemba mbali ya washambuliaji Mrisho Ngassa, Samatta na Ulimwengu.
        Hata hivyo, bado kuna wasiwasi kocha anaweza akaanza na Athumani Iddi ‘Chuji’ badala ya Kiemba kulingana na mwenendo wa mazoezi ya jana.
        Wachezaji wanaotarajiwa kuwa hazina katika mchezo wa leo ni Ally Mustafa ‘Barthez’, Mwadini Ally, Nadir Haroub, Vincent Barnabas, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco, Mudathir Yahya, Zahor Pazi, Simon Msuva, Haroun Chanongo, Mwinyi Kazimoto na Kiemba au Chuji.  
        Mchezo wa leo unatarajiwa kuanza majira ya saa 3:00 kwa saa za huku na saa 5:00 kwa saa za Tanzania.  
        Stars itaingia uwanjani ikiwa katika hali ya wasiwasi kutokana na kufanyiwa vurugu na kuzimiwa taa jana ili ishindwe kufanya mazoezi kwenye Uwanja huo siku moja kabla ya mchezo kwa mujibu wa sharia za FIFA. 
        Sheria za FIFA zinasema timu mgeni, itapewa fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja utakaotumika kwa mechi dhidi ya wenyeji katika muda ambao mechi itachezwa, lakini jana msafara wa Stars ulipofika Uwanja wa Marakech ulizuiwa kuingia ndani na askari wa uwanjani hapo. 
        Juhudi za Kocha wa Stars, Kim Poulsen kuwaelewesha askari wa Uwanja huo sheria ili wairuhusu timu kuingia uwanjani hazikuzaa matunda na ikabidi viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waingilie kati, nao pia wakachemsha.
        Ikawadia zamu ya viongozi wa Kamati ya Ushindi ya Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premum Lager, ambao nao walichemsha- ndipo baadhi wa Watanzania waishio hapa na wachache waliosafiri kutoka Dar es Salaam walipoongeza nguvu.
        Mabosi; Kutoka kulia Michael Mukuza mwakilishi wa wadhamini wa Stars, Kilimanjaro Premium Lager, Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani, Mbunge Zitto Kabwe, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Dk Amos Makalla na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Stars, Sk Ramadhan Dau 

        Walikwenda kufungua geti kwa nguvu, wakawaweka kando askari waliokuwa wanawazuia na kuiingiza timu uwanjani kufanya mazoezi. 
        Hata hivyo, Stars ilipofika uwanjani ililazimika kusubiri tena, kwani wenyeji Simba wa Atlasi walikuwa wakiendelea na mazoezi.
        Baada ya nusu saa, Morocco walimaliza awamu yao na Stars wakaanza kupasha misuli moto. Hata hivyo, baada ya dakika 34, taa za Uwanja huo zilizimwa na uwanjani kuwa giza totoro, lakini viongozi wa TFF wakaenda kuomba, zikawashwa na timu ikafanya mazoezi kwa dakika 10 zaidi na kwenda kupumzika katika hoteli ya Pullman walipofikia. 
        Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo leo itakuwa ugenini ikimenyana na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
        Stars ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki moja na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya bila mabao.
        Kabla ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa hotuba nzuri. Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
        • Blogger Comments
        • Facebook Comments
        Item Reviewed: KIM POULSEN AWAANZISHA PAMOJA NGASSA, SAMATTA NA ULIMWENGU DHIDI YA MOROCCO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry