Kulikoni Nahodha? Juma Kaseja anakwepa kwenda ofisini kwa Hans Poppe kuzungumzia Mkataba mpya |
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba Nahodha wa klabu hiyo, Juma Kaseja yeye mwenyewe ndiye anachelewesha hatima ya mustakabali wake katika klabu hiyo, kutokana na kutokuwa tayari kuzungumzia Mkataba mpya.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Poppe alisema kwamba alikwishazungumza na Kaseja na kumuelezea nia ya klabu kutaka kuendelea naye kiasi cha wiki mbili zilizopita.
Poppe alisema kwamba pamoja na kumuambia hivyo Kaseja, akamtaka atoe mapendekezo yake kuhusu Mkataba mpya, lakini kipa huyo akasema hayuko tayari kwa wakati huo.
Mpunga wa Juma upo droo ya kwanza tu hapa; Hans Poppe anasema Kaseja ndiye anajichelewesha kwa kutofika ofisini kwake wamalize suala lake |
“Kwa nia nzuri tu, alisema hayuko tayari hadi kwanza amalize majukumu ya timu ya taifa, mimi nikamuambia basi sawa. Maliza majukumu haya, ukiwa tayari wakati wowote njoo tukutane tuzungumzie suala lako,”alisema Poppe.
Hata hivyo, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kwamba hadi sasa Kaseja bado hajatokea mezani kwake kwa ajili ya kujadili Mkataba wake mpya.
“Sisi tunamuheshimu sana Kaseja, akiwa kama mchezaji wetu mwandamizi na Nahodha wa timu. Huwa hatuzungumzii naye kama ambavyo tunazungumza na wachezaji wengine, yeye huwa tunampa heshima yake kwa kuzungumza naye kwa staili ya aina yake,”alisema Poppe.
Poppe amesema hawana wasiwasi na Kaseja na wanaheshimu alichokisema, hivyo wanamsubiri, wakati wowote akiwa tayari na kutokea wataketi naye mezani kujadili naye Mkataba mpya.
Ushauri kidogo? Kipa wa Yanga Ally Mustafa Barthez amekuwa rafiki mzuri wa Kaseja hivi sasa...atakuwa anamshauri nini kuhusu mustakabali wake na Simba SC? |
Kaseja aliyejiunga na Simba SC mwaka 2003 akitokea Moro United ya Morogoro, kabla ya mwaka 2009 kuhamia Yanga alikocheza msimu mmoja na kurejea nyumbani Msimbazi, amemaliza Mkataba wake mwezi uliopita.
Kufuatia kumaliza Mkataba huo, kumekuwa na habari tofauti zikisemwa juu ya mlinda mlango huyo nambari moja nchini, kwamba huenda asiongezewe Mkataba, lakini kauli ya Poppe inadhihirisha bado ana nafasi ya kuendelea kupiga kazi Msimbazi.