IMEWEKWA JUNI 30, 2013 SAA 11:42 ASUBUHI
HUWEZI kukwepa kuweka jina la Zamoyoni Mogella katika orodha ya wachezaji bora kuwahi kutokea Simba SC na ukifanya zoezi hilo kwa mahasimu wao wa jadi, Yanga SC huwezi kuliacha jina la Edibily Lunyamila.
Lakini wawili hao pamoja na kuwa na heshima ya ugwiji wa klabu zao, pia walichezea klabu zote mbili, yaani Simba na Yanga.
Mwaka 1992 wakati Lunyamila anaibuka, Mogella alikuwa anaelekea ukingoni kisoka tangu aanze kucheza miaka ya 1970 mjini Morogoro.
Mwishoni mwa mwaka 1992, Lunyamila aligombewa na Simba na Yanga akiwa Biashara ya Shinyanga na hatimaye akadondoka Jangwani. Lakini wakati huo, shujaa wa zamani wa Simba SC, Mogella alikuwa hana raha na mwenye fikra nyingi, kutokana na kuvurugwa na uongozi wa klabu yake wakati huo.
Baada ya msimu mzuri wa 1992, akiiwezesha Simba SC kutetea ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Bara na Muungano, Mogella alitupiwa virago mwishoni mwa msimu.
Kweli, Mogella uwezo ulikuwa umefikia ukingoni baada ya kucheza kwa muda mrefu na kupumzika ulikuwa wakati mwafaka, lakini namna ambavyo aliachishwa soka hakuipenda.
Alikuwa anafurahi na mashabiki kila anapofunga. Watu walikuwa machizi kwa ajili yake. Waliimba kwa furaha na kutaja jina lake. Anawaachaje?
Msimu unaisha tu, anaambiwa kwaheri bila ya kupata fursa ya kuwapa mkono wa kwaheri mashabiki wake? Zile medali na mataji aliyoshinda vilikuwa vina thamani gani tena?
Kwa sababu hiyo Mogella aliamua kucheza kwa mwaka mmoja zaidi akiwa na jezi ya mahasimu, Yanga SC na huko alipata fursa ya kuwapungia mkono wa kwaheri mashabiki.
Simba SC kama wangempa fursa Mogella awapungie mkono wa kwaheri mashabiki kama walivyofanya Liverpool kwa Jamie Carragher mwishoni mwa msimu uliopita England, bila shaka leo Yanga SC isingetajwa kama klabu yake ya mwisho kuchezea, bali mambo yote yangeishia Msimbazi.
Lunyamila kadhalika, baada ya kuichezea Yanga tangu mwaka 1993, mwishoni mwa msimu wa 2002 alifanyiwa visa, vile vya akufukuzae, hakuambii toka.
Aliambiwa asaini kwa fedha kidogo sana kwa kuwa uwezo wake umeshuka, naye akaona bora kutosaini na Yanga SC chini ya kiongozi aliyekuwa na misimamo mikali, Tarimba Abbas ikamuonyesha milango ya kutokea Jangwani, wa mbele na nyuma, achague.
Lunyamila akaenda kusaini Simba ambako alicheza kwa msimu mmoja zaidi, baadaye akaenda Mtibwa Sugar kabla ya kutungika daluga zake.
Kuna vitu vidogo sana Simba SC na Yanga SC wanakosea na ni lazima ufike wakati wabadilike. Mchezaji anapofikia kiwango cha kuitwa gwiji, basi huyo ni sehemu ya historia ya timu na lazima apewe heshima yake.
Lazima Simba na Yanga zijifunze kuwalisha mapenzi ya timu zao wachezaji wao baada ya kustaafu kwa kuwapa heshima zao. Sina hakika kama Mogella ni mwanachama wa Simba SC, lakini ninajua ni mpenzi wa Simba.
Sina hakika kama Lunyamila ana kadi ya Yanga SC, lakini nafahamu ni mwana Yanga wa kulia kabisa timu inapofungwa.
Kulikuwa kuna ubaya gani, baada ya Mogella kumaliza muda wake wa kuitumikia Simba akaagwa na kukabidhiwa na kadi ya uanachama wa timu, kweli angethubutu kuhamia kwa wale wanaoitwa wapinzani wa jadi?
Au kwa Yanga na Lunyamila, tofauti ya dau haikuzidi Sh. Milioni 1, ingekuwa vema ikatumika busara ya kuzungumza naye na kumfanya amalizie soka yake Jangwani, kisha aagwe vizuri na kupewa kadi ya uanachama. Hiyo ni heshima kubwa sana zaidi ya kumpa fedha.
Katika hii dunia pamoja na fedha, lakini mwisho wa siku utu na heshima ni zaidi. Na ukimuona mtu anauza utu na heshima yake kwa ajili ya fedha, jua huyo ni fedhuli mkubwa.
Wachezaji wetu, baada ya kuzitumikia klabu zetu, timu ya taifa kwa muda mrefu, wanachohitaji ni heshima- na hiyo ndiyo faraja kubwa.
Wakati bado hatujasahau mikasa ya Mogella, Lunyamila na wachezaji wengine, kuna jipya limejitokeza kuhusu aliyekuwa Nahodha wa Simba SC, Juma Kaseja.
Simba SC imeamua kutomuongezea Mkataba Kaseja, baada ya kuitumikia klabu hiyo tangu mwaka 2003, (ukiondoa mwaka mmoja 2009, alipokwenda kuchezea mahasimu, Yanga SC) aliposajiliwa kutoka Moro United, maana yake imemtema.
Basi. Simba na Kaseja historia imefungwa. Kirahisi tu hivi, Kaseja si mchezaji wa Simba SC tena. Saa ngapi kapata fursa ya kuagana na maelfu ya wapenzi wa Simba waliokuwa wakimshangilia wakati akipangua mikwaju ya penalti na kuipa mataji timu? Inauma.
Sababu iliyotajwa na Simba SC kuamua kutomuongezea Kaseja Mkataba ni kwamba uwezo wake umeshuka na sasa anafungwa kwa urahisi, ingawa hilo mimi siamini, bali nachoweza kukubali, kwa sasa baada ya kudaka mfululizo muda mrefu, amechoka na anahitaji kupumzika kidogo ili awe fiti tena.
Pamoja na hayo, kama uongozi wa Simba SC umejiridhisha uwezo wa kipa huyo umeshuka, ulipaswa kuhakikisha unakutana naye kujadiliana naye na kumshauri juu ya namna ya kuondoka kwa heshima klabuni.
Hata kama Juma angekuwa anaamini bado anaweza kuendelea kucheza, Simba SC ingempa Mkataba wa si lazima acheze, ili uwezo wake ndiyo umpe nafasi kikosini. Kulikuwa kuna namna nzuri tu ya Juma na Simba kuachana zaidi ya hii iliyotumika.
Hata kama kuondoka klabuni, angepewa nafasi ya kuitisha Mkutano na Waandishi wa Habari kutangaza mwenyewe kujiuzulu kwa nia nzuri kuichezea timu, ili akakabiliane na changamoto nyingine sehemu nyingine, hata iwe hapa nchini.
Watu wanaamini busara ya namna hii ilitumika hata katika mabadiliko ya Waziri Mkuu wa nchi katika serikali hii ya awamu nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, kutoka Edward Lowassa hadi Mizengo Pinda. Lakini kwa mamlaka aliyonayo, JK angeweza mwenyewe kutangaza kumvua madaraka Lowassa.
Kitendo cha Juma kusoma kwenye vyombo vya habari kwamba hataongezewa Mkataba, kwa kweli kinaumiza na huu umekuwa utamaduni wa viongozi wetu kutowaheshimu kabisa wachezaji licha ya kuzipa klabu mataji na kuwapa furaha mashabiki kwa muda mrefu.
Kweli jamani uwezo wa mchezaji kushuka ni kosa la kutemwa ‘kiroho mbaya’ katika timu? Mchezaji gani duniani aliweza kudhibiti uwezo kushuka muda ulipofika na ingewezekana hivyo basi nyota kama Ronaldo Lima, Zinadine Zidane na Jay Jay Okocha tungeendelea kuwa nao uwanjani hadi leo.
Hili ni suala ambalo linamfika kila mchezaji wakati unapofika- na hata Haruna Chanongo ataisha tu, na tunamuonyesha nini kwa kumuacha Kaseja kwa staili hii? Jumapili njema.