Mbele ya kaburi la Msamba |
JAMHURI Mussa Kihwelo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Muda wa Umoja maalum wa wachezaji kwa ajili ya kusaidiana kwenye shida na raha, wakati Ally Mayay Tembele atakuwa Katibu wake na Jumapili wiki hii watafanya kikao cha kwanza cha kujipanga kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika kikao kilichofanyika baada ya mazishi ya Abadallah Msamba wiki iliyopita, mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Wajumbe wengine walioteuliwa kwenye Kamati hiyo ni Iddi Moshi, Boniface Pawasa, George Lucas, John Mwansasu na Abubakar Kombo.
Mayay ameomba wachezaji wote wa Tanzania, wanaocheza na waliostaafu wafike Jumapili Leaders Club kuanzia saa 4:00 asubuhi katika kikao hicho muhimu.
“Suluhisho la matatizo yetu ni sisi wenyewe, lazima tuungane, tushikamane na tufanye kitu cha kututambulisha. Lazima sisi wenyewe tuonyeshe mfano kwanza ndipo watu waje kutusaidia,”alisema Mayay enzi zake akiitwa Meja kwa sababu ya soka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Jamhuri au Julio alisistiza wachezaji wote hata waliocheza miaka ya 1960 kama wapo wajitokeze na kwamba huo si umoja wa wachezaji maalum, bali wachezaji wote nchini.