Taifa Stars |
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Addis Ababa mjini hapa kumenyana na Sudan ‘Mamba wa Mto Nile’ katika mchezo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA)
Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton kujiandaa na mchezo wa Kundi C dhidi ya Morocco Juni 8 mjini Marakech kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
Stars, inayodhaminiwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, katika mchezo wa leo, itawakosa wachezaji wake wawili nyota, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta ambao watakuwa wanaichezea klabu yao, TP Mazembe ya DRC katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Bila shaka John Raphael ‘Bocco’ atasimama badala ya Samatta na kipindi cha pili kocha Kim Paulsen anaweza akayahamishia majukumu ya Ulimwengu kwa Zahor Pazi au Simon Msuva, itategemea na aina ya mchezo na wapinzani.
Lakini kwa asilimia kikubwa kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwa kile kile kilichocheza na Morocco katika mchezo wake wa mwisho Machi 22 mjini Dar es Salaam; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa, Athumani Iddi, Frank Domayo, John Bocco na Amri Kiemba.
Kwenye benchi wanaweza kuwapo Ally Mustafa ‘Barthez’, Mwinyi Kazimoto, Mudathir Yahya, Simon Msuva, Zahor Pazi, Mwadini Ally, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Khamis Mcha, Vicent Barnabas na Haroun Chanongo.
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro anatarajiwa kuwaongoza Watanzania wachache waliopo nchini humo kwenda kuishangilia Taifa Stars.
Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.
Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya Samatta na Ulimwengu kujiunga na wenzao Juni 3 mwaka huu mjini Marrakech.