SILAHA kubwa ya klabu kongwe za soka nchini, Simba na Yanga ni idadi kubwa ya wapenzi iliyonao, kila klabu ikikadiriwa kuwa na mashabiki wasiopungua Milioni 5 nchi mzima.
Zinapokutana timu hizo, kila timu ikiwa na kikosi imara Uwanja wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000, Taifa, Dar es Salaam ‘hutapika’ na ndani ya zaidi ya dakika 90, kiasi cha Sh. Milioni 500 na zaidi huzalishwa.
Ni kiwango kikubwa sana cha fedha na haya ndiyo matunda ya kuwa na mashabiki wengi. Zaidi ya hapo, wapenzi wa timu hizo hutumia fursa ya mechi za timu hizo kujinufaisha kiuchumi kwa kuuza biashara zao ndogo ndogo uwanjani, kama vyakula na vinywaji.
Na kutokana na kuwa na mashabiki wengi, ndiyo maana hata Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imeamua kuwekeza katika klabu hizo kwa kuzidhamini kwa dau kubwa. Na bado, viongzi wa klabu hizi wangekuwa makini, wangeongeza idadi ya wadhamini, lakini kwa kuwa wanashindwa kushawishi makampuni zaidi, wanabakia na ngekewa yao ya TBL tu.
Lakini bado Simba na Yanga zinaweza kunufaika zaidi kutokana fursa ya kuwa na wapenzi wengi, iwapo wataitumia vizuri. Jezi za klabu ya Simba na Yanga kuziona kwenye miili ya mashabiki wa timu hizo sasa ni jambo la kawaida na zimetapakaa nchi nzima.
Lakini ajabu, viongozi wa klabu zote wanasema hawajui lolote kuhusu jezi hizo, wanaziona zinauzwa tu, zikiwa na nembo halisi ya klabu hiyo na ya wadhamini wao pia, Kilimanjaro Premium Lager, bia inayozalishwa na TBL.
Ajabu, pamoja na kusema hawajui lolote, viongozi wa klabu hizo hawajaonyesha hata dalili za kuzuia uuzwaji haramu wa jezi hizo.
Njia moja nzuri ya kuzuia uuzwaji wa bidhaa haramu ni kutambulisha bidhaa halali, lakini je, ni lini Simba au Yanga mojawapo imesema imeingiza sokoni jezi halisi kwa ajili ya mashabiki wake?
Na ni nini kinazuia kuingizwa sokoni kwa jezi halisi za timu hizo, ili mashabiki wanunue bidhaa halali na kuzinufaisha klabu zao kiuchumi? Haijulikani.
Leo Simba SC wanalalamika hawana fedha za kumlipa mshahara wa dola za Kimarekani 6,000 kocha wa kigeni hadi wakaamua kuachana na Mfaransa, Patrick Liewig, lakini tujiulize fedha hizo zinaweza kupatikana kutokana na mauzo ya jezi ngapi?
Na jezi zinauzwa, kiasi kwamba, imefikia hata inapotokea dharula kwa klabu hizo, nazo huingia mtego wa kununua jezi feki za ‘wamachinga’ zilizozagaa mitaani. Tuliona Yanga wakati wanataka kumtambulisha Mrisho Ngassa, walikwenda kununua jezi Kariakoo wakamvalisha. Tazama hiki kichekesho na tafakari ni aina gani ya viongozi waliopo kwenye klabu hizo- na je kweli ipo siku watabadilisha taswira ya klabu hizo?
Wasiwasi mkubwa hapa unaletwa na ukimya uliopo juu ya kupambana na jezi feki- pengine wanaopigwa changa la macho hapa ni wanachama tu wa klabu hizo, lakini kuna viongozi wananufaika na mradi huu na ndiyo hao wanaulinda.
Kwa sababu haiyumkiniki viongozi wa klabu ambao wanahaha juu ya namna ya kuziongoza klabu hizo kwa ufanisi wakanyamazia tu hujuma hii, lazima kutakuwa kuna mikono ya watu, tena wazito ndani ya klabu hizo, ambayo inalinda miradi hiyo.
Na hao wanaojifanya makomandoo wa klabu hizo, wakati mwingine ni wanafiki wakubwa, kazi yao kupeleka majungu na umbeya tu kwa viongozi wapewe noti, lakini hawana uchungu wowote na hizo klabu, maana kama wangekuwa na machungu na klabu zao, wangeanzia kwenye kupambana na hujuma hii.
Timu zikienda mikoani kucheza mechi zake, marobota ya jezi yanasafirishwa kutoka Dar es Salaam na yanauzwa kama ni biashara halali. Hakuna haja ya kudanganyana hapa, hili ni dili la watu na bila shaka ndiyo maana watu hutumia mamilioni yao kwenye kampeni kuhakikisha wanaingia madarakani, ili wakafanye biashara zao.
Yale yale, aliyowahi kusema baba wa taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mtu anapohonga hela ili kupata madaraka huyo ni wa kuogopa kama ukoma, lakini wanachama wa Simba na Yanga wanakaribisha ukoma ambao sasa unazitafuna klabu zao.
Hatuwezi kudanganyana hapa, mtu kama Aden Rage, Mwenyekiti wa Simba SC jinsi alivyo machachari anawezaje kukubali hujuma hii?
Si Rage, wala Yussuf Manji, Wenyeviti wa klabu hizo ambao mmoja kati yao anashindwa kuingia dili na kampuni kuchapisha jezi za mashabiki na klabu zikanufaika kiuchumi, lakini ukimya wao unaashiria nini? Majanga!
Ukitengeneza msingi imara wa uuzaji jezi za mashabiki, wenye ubunifu, unaweza hata kupata fedha za kujenga Uwanja wa klabu, kama ambavyo Rage na Manji wamewaahidi wapenzi wa klabu hizo, lakini wanashindwa kutekeleza ahadi hiyo.
Dhahiri ukimya uliopo juu ya hujuma hii, unaleta wasiwasi kwamba, kuna watu wazito ndani ya timu hizi wanahusika. Au TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) itusaidie, maana huu ni ufisadi mwingine sawa tu wa EPA. Jumatano njema.