Anatia timu Kinesi; Mwenyekiti wa kamati ya Usajili Simba SC, Hans Poppe atakuwapo Kinesi leo jioni |
MILIONEA Zacharia Hans Poppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, leo jioni ataongozana na wajumbe wengine wa Kamati yake kwenda kuhudhuria mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), aliyerejea Jumapili nchini kutoka Tunisia alipokwenda kufuatilia fedha za mauzo ya mshambuliaji Mganda, Emanuel Okwi katika klabu ya Etoile du Sahel ya huko yuko katika harakati za kuhakikisha Simba inakuwa imara msimu ujao.
Na leo atakwenda Kinesi ili kuona maendeleo ya timu kwa ujumla na wachezaji, hususan wale wapya waliosajiliwa kutoka timu mbalimbali katika kujaribu kutathmini kikosi cha msimu ujao.
Wachezaji wote kwa ujumla wa Simba SC wapo mazoezini, ispokuwa waliokuwa katika timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Uganda kwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwishoni mwa wiki.
Simba imepania kujiimarisha chini ya kocha mpya, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ baada ya kupitia msimu mbaya uliopita ikipokonywa ubingwa wa Ligi Kuu na kukosa japo nafasi ya pili ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho.
Ikiwa imepania kurejesha heshima msimu ujao, Simba inaonekana kuwa makini mno katika usajili na uuundaji mzima wa kikosi cha msimu mpya.
Tayati imekwishasajili wapya kadhaa kuboresha timu, wakiwemo kipa Andrew Ntalla, Issa Rashid, Mganda Samuel Ssenkoom, Adeyoum Saleh Ahmed na bado inapepesa macho kusaka nyota zaidi wa kurejesha heshima yake msimu ujao.