Anaweza; Dida akizuia mchomo wa Said Bahanuzi wa Yanga, huku akilindwa na beki wake, Aggrey Morris |
UWEZEKANO wa Juma Kaseja, kipa aliyetupiwa virago Simba SC kutua Yanga SC unazidi kuwa mdogo, kufuatia habari za wana Jangwani hao kumsajili, kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ kutoka Azam FC.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wameimarisha safu yao ya ulinzi kwa kumsajili Dida, aliyewahi kudakia pia Simba SC na Mtibwa Sugar.
Kleb amesema Dida anachukua nafasi ya Said Mohamed ambaye ameachwa baada ya kumaliza Mkataba wake.
Ametua; Dida tayari kwa kazi Jangwani |
“Dida ni kipa mzuri, ana uzoefu wa kutosha. Ni kipa ambaye amekuwa akikubalika mbele ya makocha wengi wa timu ya taifa hapa nchini, tumeona atatufaa na tumempa Mkataba wa Miaka miwili,”alisema Kleb.
Dida atakwenda kuwa kipa wa pili Yanga SC, baada ya Ally Mustafa ‘Barthez’ waliyekuwa naye Simba SC.
Magazeti yalianza kutabiri kwamba, baada ya Kaseja kumaliza miaka yake tisa ya kuitumikia Simba SC angekwenda kuungana tena na Barthez Yanga, ila kwa usajili huu wa Dida, wazi nafasi yake sasa ni ndogo.
Kaseja sasa kuna uwezekano akatua Azam FC, ambayo ina kipa mzoefu mmoja tu, Mwadini Ally ambaye naye dhahiri hafikii uwezo wa Tanzania One huyo.
Dili limeshindikana; Juma Kaseja kulia alitarajiwa kuungana tena na Ally Mustafa 'Barthez' (kushoto) |