Anarudi Mkwakwani; Uhuru Suleiman anatakiwa Coastal Union |
COASTAL Union ya Tanga imeendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao na tayari imesajili beki mwingine hatari, Abdi Banda huku ikiwa katika hatua za mwishoni za kukamilisha usajili wa yota wengine wawili, viungo Uhuru Suleiman na Mkenya Crispin Odula.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Coastal Union ya Tanga, Alhaj Nassor Bin Slum amesema kwamba wamempandisha Banda kutoka timu yao ya vijana na wako kwenye mchakato wa kumsajili kwa mkopo Uhuru kutoka Azam FC.
Amesema Odula aliyechezea Azam FC mwaka 2008 kabla ya kutimkia Bandari ya kwao, wamekwishafikia naye makubaliano na kiungo huyo wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars atahamia Barabara ya 13, Tanga msimu ujao.
Bin Slum amesema kwamba wanaamini kusajiliwa kwa wachezaji hao kutazidi kuimarisha Coastal ya msimu ujao, baada ya awali kusajili nyota wengine kama Haruna Moshi ‘Boban’ na Juma Nyosso kutoka Simba SC.
Makamu Mwenyekiti wa Coastal baada ya kusaini Mkataba na Abdi Banda kulia |
Mabingwa hao wa Ligi Kuu mwaka 1988, wamesema kwamba msimu ujao wanataka kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na Bin Slum amesema; “Ndiyo maana tunasajili wachezaji ambao watakuwa na msaada sana kwenye timu. Tunataka wakati 11 wanacheza, hata wale walio benchi wawe wachezaji wenye uwezo,”amesema.
Coastal inayofundishwa na Mzanzibari Hemed Morocco, inatarajiwa kuanza kujifua mapema mwezi ujao, wakati Ligi Kuu inatarajiwa kuanza mwishoni mwa Agosti mwaka huu.