IMEWEKWA JUNI 28, 2013 SAA 12: 58 JIONI
BEKI wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher haamini kama mshambuliaji Luis Suarez ataondoka majira haya ya joto.
Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Uruguay ametamka mara kadhaa tangu mwishoni mwa msimu kwamba anataka kuhamia Real Madrid kwa sababu ya kusakamwa na vyombo vya habari Uingereza.
Liverpool bado haijatamkiwa na mchezaji huyo au wakala wake juu ya mpango wa kuhamia klabu hiyo ya Hispania.
Mtambo wa mabao: Suarez alikuwa mfungaji bora wa Liverpool msimu uliopita, lakini ameshindwa kuibeba Uruguay
Ameaga: Carragher amestaafu mwishoni mwa msimu uliompita
Suarez bado yupo kwenye majukumu ya kimataifa katika Kombe la Mabara, ambako ataiongoza timu yake katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Italia Jumapili.
Lakini mara mashindano hayo yatakapofikia tamati, inatarajiwa ndiyo mijadala kuhusu mustakabali wake itachukua nafasi.
Na licha ya kelele zote za mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kusema anataka kuondoka, Carragher, aliyestaafu mwishoni mwa msimu uliopita, anabakia na matumaini kwamba klabu yake ya zamani itamtuliza mchezaji huyo aliyefunga mabao 30 msimu uliopita.
"Nafikiri anaweza kubaki. Klabu fulani kubwa zinaweza kuwa na nia naye, kwa sababu ni mchezaji wa kiwango cha juu na hicho ni kitu ambacho inabidi tukubali,' aliiambia ITV.
"Hatuwezi kulalamika juu ya hilo, tulimnunua kutoka Ajax. Alisani Mkataba majira yaliyopita ya joto na amebakiza miaka michache na natumai tutambakiza.
"Ni muhimu sana. Inawezekana alikuwa mchezaji bora katika Ligi Kuu England msimu uliopita na unatakiwa kuwabakiza wachezaji wako bora, ambavyo ndivyo alivyo,".