Na mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 17, 2013, SAA 12:00 ASUBUHI
NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zinatarajiwa kuwaka moto kesho, Jumamosi (Mei 18, 2013) kwa mpambano wa watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga. Huo utakuwa mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wakiwa tayari wamewavua ubingwa wapinzani wao wa jadi, Simba SC. BIN ZUBEIRY inaendelea kukuletea mfululizo wa makala za kuelekea pambano hilo linalobeba picha halisi ya soka ya Tanzania na leo tunahamia kwenye mchezo mzuri zaidi kuwahi kutokea kihistoria baina ya michezo iliyowahi kuwakutanisha wapinzani hao wa jadi. Endelea.
Moja ya mechi za Simba na Yanga hivi karibuni, Nsa Job akipiga tik tak mbele ya Juma Nyosso |
KUNA mechi Yanga iliifunga Simba 5-0. Kuna mechi Simba iliifunga Yanga 6-0 na ile ya mwaka jana ya 5-0. Lakini kwa mujibu wa wazoefu wa kushuhudia mechi baina ya miamba hiyo, haujawahi kutokea mchezo mkali wa Simba na Yanga kama ule wa Agosti 10, mwaka 1974.
Huo ulifanyika katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ukiwa ni mchezo wa Fainali ya Klabu Bingwa ya Taifa na Yanga wakatoka nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 2-1 baada ya dakika 120.
Mapema dakika ya 16, Adam Sabu (sasa marehemu) aliyekuwa akiitwa Gerd Muller akifananishwa na mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, aliifungia Simba bao la kuongoza ambalo lilidumu hadi kipindi cha pili.
Wakati baadhi ya watu wanaanza kuinuka kwenye Uwanja wa Nyamagana, wakiamini Simba SC imetetea ubingwa wake kwa bao pekee la Sabu, mshambuliaji aliyekuwa ana misuli ya nguvu ya kufumua mashuti makali, Gibson Sembuli (sasa marehemu pia) akaisawazishia Yanga, zikiwa zimebaki dakika tatu mchezo kumalizika, yaani dakika ya 87.
Kwa sababu huyo, mchezo ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza na katika dakika ya saba ya muda huo, mchezaji bora kabisa kuwahi kutokea katika ardhi ya Tanzania daima, Sunday Manara ‘Computer’ akaifungia Yanga bao la pili na la ushindi dakika ya 97.
Yanga ikarejesha ubingwa wake, kwa ushindi wa 2-1 katika pambano la kwanza kabisa baina ya watani wa jadi kufanyika nje ya ardhi ya Dar es Salaam.
KWA NINI PAMBANO BORA ZAIDI LA WATANI?
KATIKA kujiandaa na msimu wa 1974, Simba SC walifanya ziara ya mafunzo nchini Poland, wakati Yanga SC nao walikwenda Romania.
Lakini pia, kikosi cha Simba SC ni ambacho kilitwaa ubingwa msimu uliotangulia mwaka 1973 na pia ndicho kilitwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati mwaka 1974 pamoja na kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huo, wakatolewa na Mehallal El Kubra ya Misri, wakitoka kuwatoa Hearts Of Oak ya Ghana.
Kwa Yanga, kikosi chao kilikuwa kinaundwa na nyota wengi walioifikisha timu hiyo Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo, 1969 na 1970 mara zote ikitolewa na Asante Kotoko ya Ghana kwa mbinde- hivyo ukichanganya na mazoezi ya Poland na Romania, timu hizo zilikuwa moto.
Timu hizo ziliporejea nchini, zikakutana katika kituo cha mwaka huo cha Klabu Bingwa ya Taifa, mjini Mwanza enzi hizo ligi ikichezwa katika mtindo kama wa Kombe la Taifa, kunakuwa na kituo na makundi mawili na baadaye washindi wa makundi wanakutana katika fainali.
Simba na Yanga ziliongoza makundi yao na zikakutana katika fainali mjini Mwanza, mchezo ambao ulikuwa gumzo mno- mamia walisafiri kutoka mikoa mbalimbali kuelekea mjini Mwanza, wakiwemo wakazi wa Dar es Salaam. Mwanza ilifurika na Nyamagana hapakutosha.
Wakati huo, Simba SC kambi yao ilikuwa katikati ya Jiji la Mwanza tu, hoteli moja maarufu enzi hizo, Sukumaland wakati Yanga walikuwa wanaweka kambi yao Butimba.
Ikumbukwe katika mashindano ya mwaka huo, Simba SC ilimkosa kiungo wake mahiri, Khalid Abeid ambaye alikuwa majeruhi, lakini kwa mchecheto wa mechi hiyo, walitaka kumlazimisha kucheza, ila ikashindikana kwa sababu hakuwa fiti.
Ilikuwa mechi kali na ya ushindani na siku hiyo, mshambuliaji wa Simba SC, Saad Ali alizirai uwanjani baada ya kupigwa na mpira uliopigwa na Sembuli, akakimbizwa hospitali, ambako ilielezwa hakupata fahamu hadi siku ya pili. Mbaya zaidi, usiku ilivumishwa Saad amefariki dunia, lakini alipona.
Kuna uvumi fulani, eti sehemu ambayo aliangukia Saad paliota kichuguu ambacho miaka nenda, rudi hakipotei Nyamagana.
Aidha, mshambuliaji mwingine wa Simba SC, Willy Mwaijibe naye aligongana na kipa wa Yanga SC, Elias Michael ‘Nyoka Mweusi’ na wakaumia wote na kutoka nje. Nafasi ya Mwaijibe aliingia Adam Sekulu na nafasi ya Michael aliingia Muhiddin Fadhil.
Walioshuhudia wanasema soka ilichezwa Nyamagana Agosti 10 ya mwaka 1974, enzi hizo Simba na Yanga, Simba na Yanga kweli kuanzia wachezaji, viongozi hadi wapenzi. Hadi tunaingia katika milenia mpya, bado haijatokea mechi nyingine ya kufananishwa na hiyo.
Katika mchezo huo, vikosi vilikuwa; Yanga SC; Elias Michael/Muhiddin Fadhil, Suleiman Sanga, Boy Wickens, Hassan Gobbos, Omar Kapera, Abdulrahman Juma, Leonard Chitete, Sunday Manara, Gibson Sembuli, Kitwana Manara na Maulid Dilunga.
Simba SC; Athumani Mambosasa, Shaaban Baraza, Mohamed Kajole, Jumanne Masimenti, Omar Chogo, Omar Gumbo, Wily Mwaijibe/Adam Sekulu, Haidari Abeid ‘Muchacho’, Adam Sabu, Abdallah Kibadeni na Saad Ally/Abbas Dilunga.
Simba SC walikwenda Oman kabla ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Yanga walikwenda Uturuki- huwezi kuona dalili za kesho kupatikana Simba na Yanga bora kuliko ile ya Agosti 10, 1974. Tuheshimiane jamani.