Yanga wakishangilia ushindi wao |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 18, 2013 SAA 12:15 JIONI
SHEREHE za Yanga kutwaa taji la 24 la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zimefana jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hiyo inafuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao jadi Simba SC katika mchezo wa kufunga pazia la ligi hiyo.
Kwa matokeo hayo, Yanga inamaliza msimu wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 60, ikifuatiwa na Azam FC yenye 52 na Simba 45
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Martin Saanya wa Morogoro, aliyesaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Didier Kavumbangu dakika ya tano tu.
Kavumbangu alifunga kwa kichwa akiuwahi mpira wa juu uliopanguliwa na kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kushoto. Mpira uliozaa kona hiyo ulitokana na Simon Msuva ambaye alikuwa anachanja mbuga, lakini beki Haruna Shamte akatoa nje.
Simba ilipata nafasi ya kusawazisha dakika ya 27 baada ya Mrisho Ngassa kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Cannavaro na refa Saanya kuamuru penalti, lakini mkwaju wa Mussa Mudde ulipanguliwa na Ally Mustafa ‘Barthez’ kabla ya kipa huyo kuuchupia na kuudaka.
Kwa ujumla, Yanga ilitawala kipindi ca kwanza karibu chote ingawa mwishoni mwa kipindi hicho, kidogo Haruna Chanongo aliitia majaribioni ngome ya Yanga kama mara mbili hivi na kusababisha kona mbili mfululizo.
Kipindi cha pili, Simba SC walikianza vizuri dakika 10 za mwanzo wakipeleka mashambulizi langoni mwa Yanga kutokea pembeni, lakini safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Bara ilisimama imara kukabiliana na hatari zote.
Krosi maridadi ya Simon Msuva dakika ya 62 iliunganishwa vyema kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego’ kuipatia Yanga bao la pili. Baada ya bao hilo, Yanga sasa walianza kucheza kwa kujiamini zaidi na Simba wakionekana kucheza ili kutoruhusu mabao zaidi.
Dakika 87 ya refa alijeruhiwa wakati anakwenda kuamua ugomvi kati ya Didier Kavumbangu na Nassor Masoud ‘Chollo’ akaanguka na kutibiwa kwa dakika hadi kuinuka dakika ya 90 na kumaliza mpira baada ya sekunde kadhaa.
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, William Lucian ‘Gallas’, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Abdallah Seseme/Ranmadhani Singano ‘Messi’, Amri Kiemba/Jonas Mkude na Haruna Chanongo/Felix Sunzu.
Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza/Niaar Khalfan.