// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); YANGA SC ILIIPOTEZA 'VIBAYA SANA' SIMBA SC LEO - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE YANGA SC ILIIPOTEZA 'VIBAYA SANA' SIMBA SC LEO - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Saturday, May 18, 2013

    YANGA SC ILIIPOTEZA 'VIBAYA SANA' SIMBA SC LEO

    Hangaisha bwege; Pasi imetoka kwa Domayo kwenda kwa Niyonzima, Kiemba anateseka katikati

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 18, 2013 SAA 4:50 USIKU
    PAMOJA na ushindi wa mabao 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya mahasimu wao wa jadi Simba SC, Yanga SC pia ndiyo iliyotawala zaidi mchezo huo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Tathmini ya BIN ZUBEIRY kulingana na takwimu za mchezo, inaonyesha Yanga ilitawala mchezo kwa angalau asilimia 52 dhidi ya 48 za Simba SC.
    Katika mchezo huo, Yanga ilipiga krosi tisa langoni dhidi ya sita za Simba, mashuti sita dhidi ya matatu yaliyolenga lango, wakati wapinzani wao hao, walipiga mashuti sita nje, huku mabingwa hao wa Ligi Kuu wakipiga nje mashuti mawili tu. 
    Simba SC walipata kona moja zaidi ya Yanga, sita kwa tano, wakati kila timu wachezaji wake waliotea mara tatu. Yanga walicheza faulo nne zaidi ya Simba, yaani 14 kwa 10.
    Yanga walitoa mipira 22 waliyorusha Simba, wakati wapinzani wao hao walitoa mipira 18 tu. Ally Mustafa ‘Barthez’ pamoja na kucheza penalti ya Mussa Mudde, aliokoa hatari mbili zaidi, wakati Juma Kaseja pamoja na kufungwa mabao mawili, aliokoa hatari nne langoni mwake.
    Refa Martin Saanya wa Morogoro aliyeumudu vyema mchezo huo, alitoa kadi tatu za njano, mbili kwa Yanga alizowapa mabeki Mbuyu Twite na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, wakati kwa Simba alimpa Haruna Shamte.    
    Ushindi huo leo, umenogesha sherehe za taji la 24 la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa Yanga, kwani mashabiki wa timu hiyo waliangusha bonge la shangwe kuanzia kushangilia mabao hadi taji.    
    Kwa matokeo hayo, Yanga inamaliza msimu wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 60, ikifuatiwa na Azam FC iliyomaliza na pointi 55 na Simba 45. 
    Bao la kwanza...


    TAKWIMU ZA MCHEZO WA WATANI LEO:
    Simba SC Vs  Yanga SC
    6 Krosi 9
    3 Mashuti langoni  6
    6 Mashuti nje 2
    6 Kona 5
    3 Kuotea 3
    10 kucheza rafu 14
    22 Mipira ya kurusha 18
    4 Makipa kuokoa 3
    1 Kadi za njano 2
    48% Kumiliki mpira 52%                 

    Katika mchezo huo, ambao Saanya alisaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Didier Kavumbangu dakika ya tano tu.
    Kavumbangu alifunga kwa kichwa akiuwahi mpira wa juu uliopanguliwa na kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kushoto. Mpira uliozaa kona hiyo ulitokana na Simon Msuva ambaye alikuwa anachanja mbuga, lakini beki Haruna Shamte akatoa nje.   
    Simba ilipata nafasi ya kusawazisha dakika ya 27 baada ya Mrisho Ngassa kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Cannavaro na refa Saanya kuamuru penalti, lakini mkwaju wa Mussa Mudde ulipanguliwa na Ally Mustafa ‘Barthez’ kabla ya kipa huyo kuuchupia na kuudaka.
    Kwa ujumla, Yanga ilitawala kipindi cha kwanza karibu chote ingawa mwishoni mwa kipindi hicho, kidogo Haruna Chanongo aliitia majaribioni ngome ya Yanga kama mara mbili hivi na kusababisha kona mbili mfululizo.
    Kipindi cha pili, Simba SC walikianza vizuri dakika 10 za mwanzo wakipeleka mashambulizi langoni mwa Yanga kutokea pembeni, lakini safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Bara ilisimama imara kukabiliana na hatari zote.
    Krosi maridadi ya Simon Msuva dakika ya 62 iliunganishwa vyema kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego’ kuipatia Yanga bao la pili. Baada ya bao hilo, Yanga sasa walianza kucheza kwa kujiamini zaidi na Simba wakionekana kucheza ili kutoruhusu mabao zaidi.
    Dakika ya 87, refa Saanya alijeruhiwa wakati anakwenda kuamua ugomvi kati ya Didier Kavumbangu na Nassor Masoud ‘Chollo’ akaanguka na kutibiwa kwa dakika hadi kuinuka dakika ya 90 na kumaliza mpira baada ya sekunde kadhaa.   
    Baada ya mchezo huo, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga alitajwa kuwa mchezaji bora wa mechi na kupewa zawadi ya Sh. 100,000 na wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan,  Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza/Niaar Khalfan.
    Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, William Lucian ‘Gallas’, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Abdallah Seseme/Ranmadhani Singano ‘Messi’, Amri Kiemba/Jonas Mkude na Haruna Chanongo/Felix Sunzu.
    Katika mechi nyingine za kufunga pazia la ligi hiyo, Azam FC iliwafunga wenyeji JKT Oljoro 1-0 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, bao pekee la Seif Abdallah dakika ya 43, JKT Mgambo iliilaza 1-0 African Lyon Uwanja wa Mkwakwani, Tanga bao pekee la Fully Maganga dakika ya 22, Toto African iliilaza Ruvu Shooting 2-0 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mabao ya James Magafu dakika ya 38 na 49.
    JKT Ruvu iliilaza 1-0 Mtibwa Sugar, bao pekee la Mussa Hassan Mgosi dakika ya 88, Prisons ilifungwa 1-0 nyumbani Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Kagera Sugar, bao pekee la Paul Ngway dakika ya 90 na Polisi Morogoro iliilaza 2-0 Coastal Uwanja wa Jamhuri, mabao ya Kenny Masumbuko dakika ya 22 na Ally Shomary dakika ya 72. 
    Matokeo hayo yanamaanisha, Toto, Polisi Moro na African zimeipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC ILIIPOTEZA 'VIBAYA SANA' SIMBA SC LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top