IMEWEKWA MEI 22, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
BAADA ya kuwepo wasiwasi wa kutokufanyika uchaguzi mdogo wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wa kutafuta Rais mpya wa chama hicho, hatimaye mambo yamewekwa sawa na sasa tarehe ya uchaguzi huo imetangazwa.
Awali, wadau wa soka walipata wasiwasi kufuatia mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho kukaririwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini, akisema bayana kwamba hakutakuwa na uchaguzi mdogo na kuwa nafasi hiyo itaendelea kukaimiwa hadi Disemba mwakani wakati wa uchaguzi mkuu.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa chama hicho Amani Ibrahim Makungu ambaye alimrithi Ali Ferej Tamim aliyeachia ngazi mwanzoni mwa mwaka jana.
Tayari ZFA imeiagiza Kamati ya Uchaguzi kutaka zoezi hilo lifanyike terehe 8 Juni mwaka huu, ambapo Mei 17, ilikuwa siku ya kwanza kwa wanaotaka kuwania nafasi hiyo, kwenda kununua fomu katika ofisi za kamati zilizoko uwanja wa Amaan kwa Unguja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Pemba.
Katika miezi ya hivi karibuni, tulishuhudia vikao mfululizo kati ya Waziri mwenye dhamana ya michezo na wadau wa soka nchini wakiwemo maveterani, ambao walimuomba Waziri atafute njia yoyote ya kuuvunja uongozi wa sasa wa ZFA.
Sababu kubwa iliyowafanya wadau hao kushindikiza kuvunjwa kwa uongozi huo, ni madai kwamba umeshindwa kukidhi matarajio ya kulipeleka mbele soka la Zanzibar na kwamba ndio chanzo cha kuporomoka kwake.
Aidha, wamedai kuwa, viongozi hao wapo kwa ajili ya maslahi binafsi tu lakini si kwa kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Wakati akisikiliza malalamiko ya wadau hao Unguja na Pemba, Mheshimiwa Waziri aliahidi kuushughulikia ushauri wao, na kwamba kwa pamoja kati ya wizara na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), wataangalia namna bora ya kujenga taswira mpya ya mpira wa miguu nchini.
Ingawa uamuzi wa Wizara umechelewa kinyume na matarajio ya wadau, tunatumai uchaguzi mdogo wa Juni 8, ni fursa nzuri kwao kujitokeza kuchukua fomu za kugombea urais ambayo ndiyo ngazi ya juu katika safu ya uongozi wa ZFA Taifa.
Haitakuwa busara kwa wadau hao kukaa nje ya ulingo wakipiga kelele kuikosoa ZFA, lakini unapofika wakati wa uchaguzi wakawa wanaogopa kuchukua fomu kwa madai kwamba chama hicho tayari kimeandaa wagombea wao.
Ingawa kwa namna mambo yanavyoendeshwa ndani ya chama hicho, huenda ikawa ni kweli kuna mtu ameandaliwa, na kwa hivyo hata wapiga kura ambao hawajabadilika nao wakatengenezwa ili kumpitisha ‘mtu wao’, lakini ni vyema wadau waingie ili wakapambane naye.
Yumkini wadau hawana tatizo kama ZFA itaweka ‘mtu wake’ miongoni mwa wajumbe wa kamati tendaji, lakini kama hili litafanyika, ndipo ile sura kwamba chama hicho hakitaki watu wengine walio nje ya kamati zake kupenya na kushika nafasi za uongozi.
Na iwe iwavyo, bado haitakuwa busara kwa wadau hao kuogopa kivuli na kujiweka kando, huku wakiiachia nafasi hiyo igombewe na mtu mmoja, na baada ya kushinda warushe madongo wakiwa nje ilhali fomu za kugombea walizikimbia.
Kama hali itakuwa hivyo, wadau hawatakuwa na haki ya kuendelea kupiga tarumbeta baada ya chama hicho kupata Rais, aliyesimama peke yake ulingoni, kwani mwanzo wa mabadiliko yanayotafutwa, ni kuthubutu.
Ni lazima wadau wawe na uthubutu wa kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na mengine yatajulikana mbele ya safari.