Na Mahnmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 28, 2013 SAA 9:00 ALASIRI
KLABU za Azam FC, Simba SC na Yanga SC zinaweza zikalazimika kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni katika vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao kutoka watano hadi watatu, iwapo kikao cha pamoja kati ya Klabu za Ligi Kuu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kitaafiki kanuni mpya, iliyofikiwa katika Azimio la Bagamoyo miaka mitatu iliyopita.
Ilikubaliwa katika Azimio la Bagamoyo lililohusisha na viongozi wa klabu pia, kwamba kuanzia msimu wa 2013/2014 klabu zisisajili zaidi ya wachezaji watatu wa kigeni, lakini akizungumza na BIN ZUBEIRY leo mchana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah Malabeja amesema kwamba watakaa kwanza na Klabu kujadili suala hilo, ili kupata maoni yao.
Yupo hadi 2015; Haruna Niyonzima amesaini mkataba mpya hivi karibuni hadi 2015 |
“Lazima tukae kwanza na klabu ili tupate maoni yao. Kwa sababu ilikuwa tuanze mapema tu kutumia sheria hiyo, lakini klabu zikaomba katika Azimio la Bagamoyo tuanze msimu wa 2013/2014,”alisema Osiah.
Haijulikani TFF itaingia na wazo gani katika kikao chake cha pamoja na klabu, lakini kama itatoa fursa kwa klabu zipige kura kuchagua kuendelea na wachezaji watano au kufuata Azimio la Bagamoyo, kuna hatari Azam, Simba na Yanga ‘zikala hasara’.
Hiyo ni kwa sababu wapinzani wao, klabu nyingine 11 hazina wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu na nyingi hazina kabisa, hivyo kama zitataka kupunguza nguvu ya vinara hao wanaotawala Ligi Kuu, zinaweza kupiga kura ya kuunga mkono Azimio la Bagamoyo.
Joackins wa Atudo wa Azam |
Ukiondoa, Azam, Simba na Yanga, klabu nyingine zinazotarajiwa kushiriki Ligi Kuu msimu ujao ni Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, JKT Oljoro, JKT Mgambo, Prisons, Rhino FC, Ashanti United na Mbeya City.
Hata hivyo, kutokana na viongozi wa klabu nyingine kati ya hizo kuwa na mapenzi na timu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga kuna hatari hata kwenye upigaji kura zikapuuza maslahi ya timu zao wanazoziwakilisha.
Azimio la Bagamoyo lilifikia makubaliano ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni, ili kutoa fursa zaidi kwa wachezaji wazawa kwa manufaa ya taifa.
Lakini kuna hatari pia, hata TFF ikazidiwa nguvu na Usimba na Uyanga na kusahau sababu za msingi za kufikia makubaliano ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano hadi watatu kuanzia msimu ujao.
Wachezaji wa kigeni kwenye kikosi cha Azam FC ni Wakenya Jaockins Atudo, Humphrey Mieno, Mganda Brian Umony, Kipre Tchetche na Kipre Balou, wote kutoka Ivory Coast.
Katika kikosi cha Simba SC, wachezaji wa kigeni ni Waganda Abbel Dhaira, Mussa Mudde, Samuel Ssenkoom na mwingine ambaye ni mshambuliaji waliye mbioni kumsajili pamoja na Mzambia, Felix Sunzu.
Mpya kabisa Msimbazi; Samuel Ssenkoom amesaini miaka miwili Simba SC |
Yanga SC wageni ni kipa Yaw Berko kutoka Ghana, beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na washambuliaji Didier Kavumbangu kutoka Burundi na Mganda Hamisi Kiiza, ambaye hata hivyo amegoma kuongeza mkataba na nafasi yake inaweza kuchukuliwa ama Kabange Twite wa Rwanda au mchezaji mwingine wa kigeni.