IMEWEKWA MEI 22, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
WIKI iliyopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kuitoa timu ya taifa, Taifa Stars kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) iliyopangwa kufanyika nchini Zambia kuanzia Julai 2 hadi 26 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah Malabeja aliwaambia Waandishi wa Habari kwamba, Stars ambayo iliingizwa katika michuano hiyo kama timu mwalikwa imejitoa kutokana na mwingiliano wa ratiba kati ya michuano hiyo na mechi za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), dhidi ya Uganda.
Alisema awali Tanzania ilithibitisha kushiriki michuano kwa matarajio kwamba Uganda ingekubali ombi la TFF la kubadilisha ratiba ya mechi za CHAN, lakini Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) likagoma kwa vile kipindi ambacho kilipendekezwa lenyewe litakuwa na uchaguzi wa viongozi wao.
Taifa Stars itacheza na Uganda, The Cranes katika mechi za CHAN, ya kwanza ikichezwa Dar es Salaam kati ya Julai 12 na 14 mwaka huu wakati ya marudiano yatafanyika Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Kujitoa huko kwa Stars katika michuano hiyo, kulimsikitisha hata Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ambaye alisema angependa kushiriki michuano hiyo kwani ingekuwa kipimo kizuri kwa kikosi chake, lakini kwa sasa malengo makubwa ya Stars kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo fainali zake zitafanyika mwaka 2015.
Wiki kadhaa kabla ya tamko la TFF kuitoa Stars COSAFA, Mdenmark huyo, Pouslen aliunda kikosi cha wachezaji 30 wa timu ya pili ya taifa, Young Taifa Stars, ambacho alisema atakitumia kuangalia wachezaji ambao baadaye anaweza kuwajumuisha kwenye timu ya kwanza, A.
Alisema timu hiyo ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliozinduliwa Aprili 4, mwaka huu ukilenga kuwaendeleza wachezaji hao aliowateua.
Alisema timu hiyo inajumuisha wachezaji ambao wamepita umri wa kuchezea timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na wakubwa ambao hawajapata fursa ya kuingia Taifa Stars, lakini atatumia Young Taifa Stars kuangalia uwezo wao.
“Timu hii ni kiungo kati ya vijana na wakubwa. Wengi wa wachezaji watakuwa vijana, lakini wakubwa wachache watapata fursa ya kuwemo ili kuangalia uwezo wao hata kama uko nyuma waliwahi kuchezea Taifa Stars. Lakini timu hii vilevile ni changamoto wa wachezaji wa Taifa Stars kuwa wapo wanaosubiri wazembee ili wachukue nafasi zao,” alisema.
Young Taifa Stars yenye wachezaji 30 iliweka kambi ya siku tano katika hoteli ya Sapphire Court mapema mwezi huu Dar es Salaam ikifanya mazoezi Uwanja wa Karume, na baada ya hapo baadhi ya wachezaji wakapandishwa timu A, ambayo sasa ipo kambini ikijiandaa kwenda kumenyana na Morocco.
Wachezaji wa timu hiyo ni Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ali Mustapha ‘Barthez’ (Yanga) ambao ni makipa. Mabeki ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily Mgeta (Simba).
Viungo ni Haruna Chanongo (Simba), Edward Christopher (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), William Lucian (Simba), Jonas Mkude (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Abdallah Seseme (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Farid Mussa (Azam) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (JKT Ruvu), Twaha Hussein (Coastal Union), Seif Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar).
Ukirejea maelezo ya kocha Kim kuhusu kuunda timu hiyo, kwamba anataka aitumie kama daraja kati ya timu ya vijana na ya wakubwa, Taifa Stars ili kuwaendeleza wachezaji aliowateua, huoni kwa nini TFF iliitoa timu COSAFA, wakati kuna Young Taifa Stars.
Kuwepo kwa Young Taifa Stars, maana yake Tanzania sasa ina timu mbili za taifa- na ukizingatia baadhi ya wachezaji wa timu A, ambao wanacheza nje kama Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu hawaruhusiwi kucheza CHAN.
Kulikoni kuitoa timu hiyo kwenye mashindano hayo, ni bora Kim angegawa vikosi viwili kutokana na timu hizo mbili, moja icheze mechi za kufuzu za CHAN dhidi ya Uganda na nyingine iende COSAFA, ikiongozwa na Samatta na Ulimwengu.
Michuano ya COSAFA ni mikubwa na inashirikisha nchi nyingi ambazo kwa hakika zimetuacha kisoka- hivyo si vijana wa Young Taifa Stars pekee, bali hata akina Samatta na Ulimwengu ingewasaidia mno kuimarisha viwango vyao na kuja kuisaidia zaidi Taifa Stars katika kampeni za kufuzu kwenye Kombe la Dunia mwakani.
Lakini ajabu yakatoka majibu ya haraka, Tanzania inajitoa bila hata kutafakari kwa kina juu ya fursa ambayo wanaitupa. Kupata michezo ya kujipima nguvu dhidi ya timu za COSAFA, unazungumzia nchi kama Msumbiji, Zimbabwe, Zambia, Angola na Afrika Kusini hakika si fursa ya kukubali kuipoteza kwa urahisi, tena ukizingatia yatakuwa mashindano maalum.
Mara kadhaa katika michuano ya CECAFA, hualikwa timu za ukanda mwingine zikiwemo kutoka huko COSAFA kama Zambia au Magharibi imekwishakuja Ivory Coast, lakini hawakuja na vikosi vyao vya kwana kabisa, bali timu za pili. Hawa akina Kipre Tchetche na Kipre Balou wanaocheza Azam hivi sasa ni matunda ya Kombe la CECAFA Challenge mwaka 2010 mjini Dar es Salaam, walikuja na Ivory Coast.
Felix Sunzu anayecheza Simba SC kwa sasa ni matunda ya Challenge ya 2010 pia, alikuja na Zambia- sasa kulikuwa kuna ugumu gani nasi kuipeleka Young Taifa Stars yetu COSAFA, tena ikiongezewa nguvu na Samatta na Ulimwengu ambao hawatacheza CHAN? Nawasilisha na ninainuka. Tukijaaliwa Jumapili tena hapa hapa kama kawaida.