IMEWEKWA MEI 30, 2013 SAA 3:45 ASUBUHI
MSHAMBULIAJI Luis Suarez amezua hofu juu ya mustakabli wake katika klabu ya Liverpool baada ya kusema itamuwia vigumu kukataa ofa ya Real Madrid.
Suarez, anayetumikia kifungo cha adhabu ya mechi 10 kwa kumng'ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic, amesema katika mahojiano na kituo cha Redio cha Uruguay analazimika kuondoka kutokana na jinsi anavyoshambuliwa na vyombo vya habari England.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema: "Liverpool wanataka nibaki, lakini ngumu kuwakatalia Real Madrid.
Mtikisiko: Suarez amesema itakuwa ngumu kuikatalia Real Madrid
"Nina familia ambayo pia inaathiriwa na hali hii na imevuka kiwango.
"Sijiandai kupambana na Waandishi wa Habari wa England. Nimepambana sana tangu nikiwa mdogo kufika hapa nilipo, kuwaacha waandishi fulani wanitendee ubaya.
"Hawanihukumu kama mimi ni mchezaji, bali mtazamo wangu. Wananizungumzia kana kwamba wanafahamu maisha yangu yote vizuri. Nina mke na mtoto wa kike na siko tayari kuendelea kupambana na vyombo vya habari vya England,"alisema.
Liverpool imesistiza Suarez hauzwi na kwamba kwa kuwa alisani mkataba mpya wa miaka minne msimu uliopita, wanatarajia atabaki.
Suarez kwa sasa yupo na timu yake ya taifa, Uruguay
Kocha Brendan Rodgers hana presha ya kumuuza mchezaji huyo, lakini Madrid wanaandaa Pauni Milioni 25 na wachezaji wawili, washambuliaji chipukizi Alvaro Morata na Jese Rodriguez.
Liverpool pia inakabiliwa na mtihani wa kumzuia kipa Pepe Reina anayetakiwa Barcelona ambaye amesema wazi itakuwa vigumu kukataa ofa ya vigogo wa Catalan.
"Ni vigumu kuwakatalia Barca, pamoja na kwamba sina uhakika kama wananihitaji kwa dhati,' alisema mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 30.
Aspas amefanya vizuri katika msimu wake huu wa kwanza La Liga
Lakini Liverpool imeimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kukubali kumsajili kwa Pauni Milioni 6, mshambuliaji wa Celta Vigo, Iago Aspas, mwenye umri wa miaka 25, ambaye anaweza kucheza katikati au pembeni.
Huku Celta Vigo ikikabiliwa na hatari ya kushuka Daraja dau hilo ni punguzo kutoka Pauni Milioni 8 na Aspas atafanyiwa vipimo vya afya wiki ijayo.