Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal akimpa pole mjane wa marehemu Sykes |
Na Ezekiel Kamwaga, IMEWEKWA MEI 20, 2013 SAA 6:00 USIKU
MWENYEKITI wa klabu ya soka ya Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage (Mb), kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya Simba, Wapenzi na Wanachama wa klabu anapenda kutoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa aliyekuwa mdhamini wa Simba, Mzee Ally Kleist Sykes (86) aliyefariki dunia juzi jijini Nairobi, Kenya.
Mzee Sykes, mmoja wa wadhamini wa muda mrefu wa Simba, alikwenda Nairobi kwa matibabu na Rage amesema msiba huu ni pigo kubwa sana kwa klabu.
“Kwa watu ambao wameifahamu Simba kwa muda mrefu, watafahamu namna Mzee Sykes alivyokuwa msaada mkubwa wa hali na mali kwa klabu. Tangu mambo ya wafadhili hayajaanza, yeye alikuwa baadhi ya watu waliokuwa wakiisaidia Simba kwa moyo wao wote. Aliteuliwa kuwa mdhaamini kutokana na busara zake, mapenzi yake kwa klabu na uadilifu aliokuwa nao,” alisema Rage.
Ally Kleist Sykes alizaliwa mnamo Septemba 10, mwaka 1926 jijini Dar es Salaam. Alikuwa miongoni mwa watoto watatu wa kiume wa Mzee Kleist Sykes; miongoni mwa waasisi wa chama cha TAA ambacho baadaye kilikuja kujulikana kama TANU kilicholeta uhuru wa Tanganyika (TANZANIA). Kaka zake wengine ni Abdul Wahid (marehemu) na Abbas.
Kutokana na msiba huo, Rage amesema Simba inatoa ubani wa kiasi cha Sh milioni moja.
Majina ya akina Sykes hayana asili ya kawaida ya majina ya kibantu kwa vile walikuwa na asili ya kabila la Wazulu kutoka Afrika Kusini.
Mzee Sykes amezikwa leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar ambapo marehemu baba na kaka yake walizikwa.