IMEWEKWA MEI 19, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara limefungwa jana kwa mechi saba kuchezwa kwenye viwanja tofauti nchini, kubwa na iliyoteka hisia za wengi ni ile iliyowakutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Mrundi, Didier Kavumbangu kipindi cha kwanza na Mganda, Hamisi Kiiza kipindi cha pili. Ni desturi ambayo tumeizoea sasa, kila baada ya mechi ya watani, timu inayofungwa huanza kutafuta sababu za kupoteza mchezo.
Si mbaya, ni mfumo wa kawaida kwa timu kuangalia sababu za kufungwa, lakini mbaya tu kwa hapa kwetu, hazitazamwi sababu za kiufundi, kumekuwa na desturi ya kuwatafatuta wa kuwabebesha lawama na baadaye kuwatoa kafara.
Waathirika wakubwa huwa ni wachezaji na walimu wakati mwingine- wakidaiwa kuhujumu timu. Ni kosa Simba na Yanga kufungwa baina yao na ikitokea hivyo basi hujuma.
Lakini ukienda kwenye mfumo mzima wa maandalizi ya mechi hizi mambo mengi hufanyika- ikiwemo imani za kishirikina. Waganga hupewa fedha watengeneze ushindi, lakini unapokosekana ushindi, wao huwa hawabebeshwi lawama, hata kama klabu ilitimiza yote iliyoagizwa na mtaalamu wake.
Mimi si muumini wa hayo mambo na nitazidi kumuomba Mungu, daima ‘La ilaha illa Llah’ ienedelee kuwa kinga na tiba yangu, lakini kwa kutambua wajibu wangu mbele ya jamii, napaswa kuyazungumzia mambo haya, kwa sababu yapo.
Hatukuona staili waliyotumia Simba SC kuingia uwanjani? Ilikuwa ni fasheni ya kusalimu mashabiki kwenda kukizunguka kile kibendera, au? Sasa timu imefungwa na kama yale yalikuwa maagizo ya mtaalamu, wamgeukie sasa na wahoji mbona miiko imefutwa na wamefungwa?
Soka ni mchezo wa kitaalamu na ina misingi yake, taratibu zake, kanuni, sheria na ustaarabu rasmi pia. Mambo matatu ndio msingi mkuu wa soka; kushinda, kufungwa au kutoa sare na kwa yeyote anayetaka kuwa sehemu ya familia ya mpira wa miguu, lazima awe tayari kukubaliana na haya.
Lakini, pamoja na ukweli huo, bado tathmini za kwa nini matokeo fulani yametokea zinaweza kuendelea kufanyika, ila tu ziwe za kitaalamu na kiufundi- na hivyo ndivyo ilivyo dunia nzima.
Ajabu, si kwetu Tanzania. Baada ya kipigo cha jana Simba SC kutoka kwa watani, muda si mrefu zitaanza tuhuma dhidi ya wachezaji wamehongwa, wamecheza chini ya kiwango, na inawezekana wengine wakatolewa kafara.
Mara nyingi hii huwa ni kwa ajili ya viongozi kujikosha, lakini kwa nini wajikoshe wakati kufungwa ni sehemu ya soka? Lazima umefika wakati tuondokane na utamaduni huu usio na maana wala tija katika soka yetu na tuupe heshima yake mchezo huu, kwa kuwa tayari kukubaliana na matokeo, kwani huo ndiyo uungwana, kama isemavyo kaulimbiu ya FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), Fair Play.
Ukiniuliza kwa nini Simba SC walifungwa, nitakuambia walizidiwa. Na kweli walizidiwa. Lakini bado na wao walicheza vizuri kadiri ya uwezo wao na walitengeneza nafasi ambazo walishindwa kuzitumuia ikiwemo penalti, wakati wakiwa nyuma kwa 1-0.
Waingereza walisema, soka ni mchezo wa bahati. Na Mussa Mudde si mchezaji wa kwanza kukosa penalti. Wamekosa penalti wachezaji bora duniani na mafundi kweli, kama Zinadine Zidane, Rivaldo Ferreira na hata Cristiano Ronaldo.
Miongoni mwa wachezaji wa Tanzania waliokuwa mafundi wa kupiga penalti enzi zao ni Hussein Amaan Marsha- naye aliwahi kukosa. Wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 Afrika Kusini, Asamoah Gyan ndiye alikuwa anaaminiwa kwa kupiga penalti, lakini alikosa penalti muhimu dhidi ya Uruguay katika Robo Fainali.
Unaweza kuona hupaswi kumlaumu Mudde. Kwa ujumla huu haukuwa msimu mzuri kwa Simba na haya ni matunda ya migogoro waliyoipa nafasi muda mrefu, ambayo kwa kiasi fulani iliwavuruga hata wachezaji kisaikolojia.
Sasa basi, vema Simba wakajizuia kabisa kutafuta mchawi na badala yake, waangalie walijikwaa wapi, kisha wajipange kwa sababu soka inaendelea na mwisho wa msimu mmoja ni mwanzo wa maandalizi ya msimu mwingine. Nimefika.