Wachezaji wa Taifa Stars, Athumani Iddi 'Chuji' mbele na Mbwana Samatta nyuma mazoezini |
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limemteua refa kutoka Afrika Kusini, Fraser Daniel Bennett kuchezesha mechi ya Kundi C, kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwakani Brazil, kati ya Tanzania, Taifa Stars na wenyeji Morocco, Simba wa Atlasi.
Mechi hiyo itachezwa Juni 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Grand mjini Marrakech, Morocco kuanzia saa 3:00 usiku kwa saa za Morocco na saa 5:00 kwa saa za Tanzania.
Bennett atasaidiwa na Thusi Zakhele Siwela pia wa Afrika Kusini, wakati msaidizi namba mbili atakuwa ni Marwa Range kutoka Kenya. Refa wa akiba (fourth official) ni Lwandile Mfiki wa Afrika Kusini pia.
Kamisaa wa mechi hiyo ni Robert Mangollo-M’voulou wa Gabon wakati mtathimini wa waamuzi (referee assessor) ni Charles Masembe kutoka Uganda.
Taifa Stars ambayo iko chini ya Kocha Kim Poulsen, na ikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikiendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo ambapo kabla itajipima na Sudan (Nile Crocodiles) Juni 2 mwaka huu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Hadi sasa, Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza tatu kushinda mbili na kufungwa moja, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, iliyoshinda mechi mbili na kutoa sare moja.
Kama Stars itashinda ugenini dhidi ya Morocco, itajiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Brazil, kwani ikiongoza Kundi hilo, itacheza mechi mbili za mwisho nyumbani na ugenini dhidi ya moja ya timu zilizoongoza makundi ambayo ikishinda itaweka historia ya kucheza Fainali za Kwanza za Kombe la Dunia.
Stars inayonufaika na udhamini wa bia ya Kilimanjaro, imekuwa na mwenendo mzuri chini ya Mdenmark Kim Pouslen, ambaye ameiwezesha kushinda mechi tano kati ya 10, sare tatu na kufungwa mbili tangu aanze kazi Mei mwaka jana, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.Kikosi cha Stars kilichopo kambini kinaundwa na makipa; Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na Salum Abubakar (Azam).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).
Kocha Kim amesema kikosi kitakachoingia kambini kitakuwa na wachezaji 24 ambapo Samata na Ulimwengu watajiunga na timu jijini Marrakech, lakini wachezaji atakaondoka nao Dar es Salaam kwenda Addis Ababa ni 22 ambapo ataacha kipa mmoja na mchezaji mmoja wa ndani.
Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.
Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.