Rais Kikwete akiwa na Tenga juzi Ikulu |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 25, 2013 SAA 1:30 ASUBUHI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujenga uwezo wa kuwalipa makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, ili Serikali ijivue mzigo huo.
JK akiagana na Tenga juzi |
Akizungumza Ikulu mjini Dar es Salaam juzi, Rais Kikwete alisema kwamba Serikali imelazimika kuendelea kulipa mishahara ya makocha wa timu ya taifa, kwa sababu bado TFF hawana uwezo wa kufanya hivyo.
Hata hivyo, Rais Kikwete alimtaka Rais wa TFF, Leodegar Chillah Tenga kuhakikisha wanajenga uwezo wa kulipa maocha wa timu hiyo na kuipunguzia mzigo huo Serikali.
Rais Kikwete alianza kugharamia mishahara ya makocha tangu alipoingia Ikulu mwaka 2005 na mwalimu wa kwanza alikuwa ni Mbrazil Marcio Maximo aliyeanza kazi Juni mwaka 2006 nchini, akafuatiwa na Mdenmark, Jan Borge Poulsen mwaka 2010 na sasa Mdenmark mwingine, Kim Poulsen aliyeanza kazi Mei mwaka jana.
Rais pia alimpongeza Kocha Poulsen kwa kuifikisha Stars sehemu nzuri katika kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil na akamtaka kuongeza bidii kuhakikisha anaendeleza wimbi la ushindi.
Rais Kikwete aliwaalika wachezaji wa Stars chakula cha mchana Ikulu mjini Dar es Salaam juzi na akawaahidi kuwafanyia jambo zuri iwapo watamaliza wanaongoza Kundi C.
Wachezaji waliokuwapo Ikulu juzi ni makipa; Nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Mudathiri Yahya (Azam).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).
Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC, hakuwepo Ikulu juzi kutokana na kufiwa na baba yake mlezi, wakati Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, wanaochezea TP Mazembe ya DRC, wataungana na timu Marakech ambako Stars itakwenda kumenyana na wenyeji Morocco Juni 8 katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili kwenye kundi hilo, lenye timu za Ivory Coast na Gambia pia.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, imeweka kambi katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikiendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo ambayo itatanguliwa na mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Sudan, Nile Crocodiles Juni 2 mwaka huu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Rais Kikwete akiwa na wachezaji wa Stars na kocha Kim juzi Ikulu |
Hadi sasa, Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza tatu kushinda mbili na kufungwa moja, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, iliyoshinda mechi mbili na kutoa sare moja.
Kama Stars itashinda ugenini dhidi ya Morocco, itajiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Brazil, kwani ikiongoza Kundi hilo, itacheza mechi mbili za mwisho nyumbani na ugenini dhidi ya moja ya timu zilizoongoza makundi ambayo ikishinda itaweka historia ya kucheza Fainali za Kwanza za Kombe la Dunia.
Stars, imekuwa na mwenendo mzuri chini ya Mdenmark Kim Pouslen, ambaye ameiwezesha kushinda mechi tano kati ya 10, sare tatu na kufungwa mbili tangu aanze kazi Mei mwaka jana, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1, mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.
Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.
REKODI YA KIM POULSEN STARS
P W D L GF GA GD Pts
Kim Stars 10 5 3 2 13 10 3 18
Mei 26, 2012
Tanzania 0 – 0 Malawi (Kirafiki)
Juni 2, 2012
Ivory Coast 2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 10, 2012
Tanzania 2 – 1 Gambia (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 17, 2012
Msumbiji 1 – 1 Tanzania (Tanzania ilitolewa kwa penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
Agosti 15, 2012
Botswana 3 – 3 Tanzania (Kirafiki)
Novemba 14, 2012
Tanzania 1-0 Kenya (Kirafiki)
Desemba 22, 2012
Tanzania 1-0 Zambia (Kirafiki)
Januari 11, 2013
Tanzania 1-2 Ethiopia (Kirafiki)
Februari 6, 2013
Tanzania 1-0 Cameroon (Kirafiki)
Machi 22, 2013
Tanzania 3-1 Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)
MSIMAMO WA KUNDI C:
P W D L GF GA Pts
Ivory Coast 3 2 1 0 7 2 7
Tanzania 3 2 0 1 5 4 6
Morocco 3 0 2 1 4 6 2
Gambia 3 0 1 2 2 6 1