Mgambo JKT wanahitaji sare kubaki Ligi Kuu |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 17, 2013 SAA 5:10 ASUBUHI
PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa kesho, kwa nyasi za viwanja saba kuwaka moto nchini, ukiwemo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako watani wa jadi, Simba na Yanga watamenyana.
Mechi nyingine; kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wenyeji Tanzania Prisons wataikaribisha Kagera Sugar ya Bukoba, Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, JKT Oljoro wataikaribisha Azam FC ya Dar es Salaam, Jamhuri Morogoro, Polisi wataikaribisha Coastal Union ya Tanga, Azam Complex, Chamazi, JKT Ruvu wataikaribisha Mtibwa Sugar, Mkwakwani, Tanga Mgambo JKT wataikaribisha African Lyon na CCM Kirumba, Mwanza, Toto African wataikaribisha Ruvu Shooting.
Nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu zimekwishapata wenyewe na mvuto kuelekea mechi za kufunga msimu, mbali na upinzani wa jadi wa Simba na Yanga, zaidi ni katika vita ya kuepuka kushuka Daraja.
Hadi sasa katika timu zinazotakiwa kushuka, ni African Lyon pekee ambayo imejihakikishia kuipa mkono wa kwaheri ligi hiyo, lakini zaidi ya hapo timu tatu zote zinawania kuepuka balaa la kushuka ambazo ni Toto, Polisi zenye pointi 22 kila mmoja na Mgambo yenye pointi 25.
Mgambo inayocheza nyumbani dhidi ya Lyon, inapewa nafasi kubwa ya kuzipiku Polisi na Toto, kwa sababu inahitaji sare tu katika mchezo wake wa kesho, kufikisha pointi 26 ambazo haziwezi kufikiwa na timu hizo za Mwanza na Morogoro.
Lakini kama Mgambo itafungwa na Polisi na Toto zikashinda, timu ya kubaki Ligi Kuu kati ya hizo tatu itatazamwa kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hadi sasa, katika mabao ya kufunga na kufungwa, timu zote zimefungwa zaidi, Mgambo mabao 11, Polisi 10 na Toto 12. Maana yake Mgambo ikifungwa 1-0, itakuwa imefungwa 12 zaidi na kama Toto ikishinda 1-0, itabaki Ligi Kuu kwa kuwa itapunguza bao moja na kubaki 11, iwapo na Polisi haitashinda.
Lakini kama Mgambo ikifungwa 1-0 tu na Polisi ikashinda 1-0 pia, itabaki Ligi Kuu. Kwa ujumla mchuano wa kuepuka kushuka Daraja ndiyo utakaokuwa mkali zaidi kesho.