Kipepeo; Mrisho Ngassa amerejea Yanga |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 24, 2013 SAA 1:00 MCHANA
KATIKA mzunguko wote wa pili, kocha Ernie Brandts wa Yanga SC, amekuwa akimtumia kama kiungo wa pembeni Haruna Niyonzima na katikati chini, anacheza Athumani Iddi ‘Chuji’, juu yake Frank Domayo.
Niyonzima amekuwa akicheza upande wa kushoto wa Uwanja na kulia, Simon Msuva na wote wamekuwa na mchango mkubwa kwa mafanikio ya Yanga SC msimu huu.
Msuva anateleza kulia na kumimina krosi za kuzalisha mabao, wakati mwingine akifunga mwenyewe na Haruna kadhalika upande wa kulia.
Anateleza kushoto; Haruna Niyonzima akiambaa upande wa kushoto wa Uwanja |
Lakini wiki hii, Yanga SC imeongeza kiungo mwingine hodari wa pembeni, Mrisho Ngassa ambaye wazi kusajiliwa kwake sasa kutamfanya kocha Mholanzi, Brandts abadilishe mipango yake ya matumizi ya wachezaji.
Atafanyeje? Hilo ndilo swali ambalo wengi watasubiri kuona wakati Yanga itakapoanza msimu mpya.
Atamrudisha Niyonzima katikati, na vipi kuhusu Domayo ambaye ambaye ameonekana kuimudu vyema nafasi hiyo kiasi cha kuifanya safu ya kiungo ya Yanga iwe bora katika Ligi Kuu msimu huu?
Kiberenge; Simon Msuva akiteleza upande wa kulia wa Uwanja |
Au atamrudisha Domayo kucheza kama kiungo mkabaji, nafasi aliyokuwa akiicheza wakati anaingia Yanga, na vipi kuhusu Athumani Iddi ‘Chuji’ ambaye ameimudu vyema nafasi hiyo kiasi cha kutajwa mchezaji bora wa mechi dhidi ya watani, Simba Mei 18?
Na akimuacha pembeni Haruna, Ngassa atacheza wapi? Wazi kama atamuacha pembeni Niyonzima, Msuva atarudi katika benchi na kuwa mchezaji anayeingia kutokea nje.
Na maana yake, uwezekano wa Nizar Khalfan na Nurdin Bakari kuwa na namba katika kikosi cha kwanza unazidi kupungua.
Katikati; Frank Domayo na Athumani Iddi (nyuma) wamemudu nafasi ya kiungo msimu huu |
Kuingia kwa Ngassa Yanga ni faida kubwa kwa timu hiyo, kwani imeimarisha safu yake ya ushambuliaji, ikiwa na mtu mpya wa kasi na uwezo wa kufunga.
Lakini siku zote walimu ndiyo huwa wana majibu juu ya matumizi ya wachezaji, vema tumsubiri Brandts atakaporejea nchini na kuanza kuandaa timu yake kwa ajili ya msimu ujao, tuone atafanyeje?