Micho akikabidhiwa jezi namba moja ya Uganda baada ya kutangazwa katika ofisi za FUFA, Mengo leo. |
Na Israel Ojoko, Kampala IMEWEKWA MEI 21, 2013 SAA 2:00 USIKU
MAKOCHA wawili waliowahi kuifundisha Yanga SC ya Dar es Salaam kwa vipindi tofauti, Mserbia Militun Sredojevic ‘Micho’ na Mganda, Sam Timbe leo wametangazwa kuwa makocha wapya wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes.
Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) limetangaza kuingia na Micho mwenye umri wa miaka 43 mkataba wa miaka miwili leo katika ofisi zake zilizopo eneo la Mengo.
Micho aliyefukuzwa timu ya taifa ya Rwanda hivi karibuni kwa matokeo mabaya, anawapiku kocha wa zamani wa Nigeria, Super Eagles, Samson Siasia na kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet aliyewahi kufundisha Yanga.
Timbe aliyewahi kufanya kazi kama Kocha Msaidizi wa Micho, SC Villa ya Uganda, ambaye kwa sasa ni kocha wa Polisi ya nchini humo kwa pamoja na kocha wa BUL BIDCO, Kefa Kisala na kocha wa makipa, Fred Kajoba watakuwa wasaidizi wa Mserbia huyo.
Nafasi ya ukocha The Cranes ilikuwa wazi baada ya kutimuliwa kwa Msoctland, Bobby Williamson aliyeiwezesha timu hiyo kutwaa mataji manne ya Kombe la Challenge, ingawa alishindwa kuiwezesha timu hiyo kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika.
Wakati Micho alikuwa kocha wa Yanga mwaka 2007 na hakuacha kumbukumbu ya taji lolote, mwaka 2011, Sam Timbe naye aliifundisha timu hiyo ya Jangwani na kuiachia taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, likiwa la kwanza tangu walipotwaa mara ya mwisho mwaka 1999.