Na Prince Akbar, IMEWEKWA MEI 20, 2013 SAA 11:00 JIONI
VIONGOZI wawili kutoka Manchester United ya England, Anthony Benerjee, Mkurugenzi wa Uhusiano na Michael Higham, Meneja Uhusiano wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Jumatano kwa ajili ya kufanya manzungumzo na viongozi wa Airtel Tanzania kuhusu uendeshaji bora wa michuano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Airtel Rising Stars mwaka huu.
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando amesema mkutano huo utakaojumuisha wadau mbalimbali utafanyika makao makuu ya Airtel Tanzania, eneo la Morocco, Dar es Salaam na kutathimini ARS ya miaka miwili iliyopita ili kuona namna nzuri ya kuendesha michuano hiyo siku zijazo kuanzia mwaka huu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni miongoni mwa ya wadau wataoshiriki mkutano huo ili kutoa mchango wao hasa katika masuala ya
kifundi kama vile upangaji wa ratiba ya mashindano.
Ratiba ya kuanza kwa ARS 2013 inatarajiwa kutangazwa mwezi huu.
Michuano ya soka Airtel Rising Stars ilizinduliwa hapa nchini Tanzania na sehemu nyingine barani Afrika mwaka 2011 ikiwa na lengo mahsusi la kusaidia kuvumbua vipaji vya wanasoka chipukizi na kuwafanya waonekane kwa makocha na mawakala wa kusaka vipaji vya wachezaji nyota.
Mashaindano haya huanzia ngazi ya chini ambapo timu za sekondari ngazi ya mkoa huchuana ili kupata wachezaji nyota wa kuunda kombaini inayowakilisha mkoa husika kwenye mashindano ya Taifa ambayo hufanyika Dar es Salaam na jumla ya timu 48 zimepata fursa ya kushirikia ARS katika miaka miwili iliyopita.
Katika mwaka wa uzinduzi 2011 mashindano ya ARS ngazi ya Taifa, yalifuatiwa na kliniki ya kimataifa chini ya usimamizi wa makocha kutoka Manchester United iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushirikisha wavulana na wasichana kutoka nchi za Kenya, Malawi, Sierra Leone na mwenyeji Tanzania.
Mwaka jana fainali za taifa za ARS zilifuatiwa na michuano ya kimataifa ya ARS zilizofanyika jijini Nairobi zikishirikisha nchi ambazo kampuni ya Airtel hufanya biashara.
Aidha, kliniki ya mwaka jana ilifanyika Nairobi chini ya usimamizi ya makocha wazoefu kutoka shule za mafunzo ya soka ya vijana za Manchester United ambapo vijana walipata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za soka.