Kulia Allan Mapigo na kushoto Ababuu Mwana Zanziabr, miongoni mwa wanaowania tuzo ya Mtayariashaji Bora wa Bendi |
ZOEZI la upigaji wa kura za tuzo za wanamuziki bora Tanzania, maarufu kama Kilimanjaro Music Award lililoanza Mei 2, mwaka huu linazidi kupamba moto kwa wapenzi wa muziki kuwapigia kura wasanii wawapendao.
Jana kwa muhtasari tulielezea ushindani uliopo katika kipengele Mtunzi Bora wa Mashairi ya Bendi ambacho kinawashindanisha Chaz Baba, Greyson Semsekwa, Jonico Flower, Jose Mara na Khaleed Chokora.
Awali tulitazama vipengele vya Mtunzi Bora wa Hip Hop ambako wanaochuana ni Fid Q, Joh Makini, Kala Jeremiah, Mwana FA na Stamina, baada ya kutazama kipengele cha Mtunzi Bora wa Mashairi ya Bongo Fleva, tuzo ambayo inashindaniwa na Ally Kiba, Barnaba, Ben Pol, Linex na Ommy Dimpoz.
Tayari tumetazama pia vipengele vya Mtunzi Bora wa Mashairi ya Taarab, wanapokutana Ahmed Mgeni, Hemed Omary, Khadija Kopa, Mzee Yussuf, na Thabit Abdul, Video ya Wimbo Bora wa mwaka, tuzo inayowaniwa na Ommy Dimpoz kupitia wimbo Baadae, Profesa Jay na Marco Chali wimbo Kamili Gado, Rich Mavoko na wimbo Marry Me, Bob Junior na wimbo Nichumu na AY na Marco Chali katika wimbo Party Zone.
Tumetazama pia vipengele vya Msanii Anayechipukia, ambako Ally Nipishe anachuana na Angel, Bonge la Nyau, Mirror na Vanessa Mdee, Msanii Bora wa Hip hop ambacho kinawashindanisha Fid Q, Joh Makini, Kala Jeremiah, Profesa Jay na Stamina.
Tumetazama pia kipengele cha Msanii Bora wa Kiume na wa kike wa Bendi, ambako Kwa wanaume, Chaz Baba anachuana na Dogo Rama, Greyson Semsekwa, Jose Mara na Khaleed Chokora na kwa wanawake Anneth Kushaba anachuana na Luiza Mbutu, Mary Lucos na Vumilia.
Katika mfulululizo huu, tayari tumejadili pia vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike Bongo Fleva, ambako kwa wanaume, Ally Kiba anachuana na Ben Pol, Diamond, Linex na Ommy Dimpoz, wakati kwa wanawake Linah anapambana na Mwasiti, Recho na Shaa.
Tumetazama pia kwa Msanii Bora wa Kiume na wa Kike Taarabu, ambako Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Khadija Yussuf na Leila Rashid wanawania Umalkia na akina Ahmed Mgeni, Hashim Said na Mzee Yussuf wanapigania Ufalme.
Msanii Bora wa Kiume na wa Kike kwa ujumla, ambavyo vinawashindanisha Ben Pol, Diamond, Linex, Mzee Yussuf na Ommy Dimpoz kwa ‘wakaka’, wakati Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Lady Jaydee, Mwasiti na Recho watawania tuzo ya Msanii Bora wa Kike na wimbo bora wa mwaka ambako Rapa Kala Jeremiah, kupitia wimbo wake Dear God anachuana na kundi la Kigoma All Stars na wimbo wao Leka Dutigite, Mwasiti aliyemshirikisha Ally Nipishe katika wimbo Mapito, Ommy Dimpoz aliyemshirikisha Vanessa Mdee katika wimbo Me n U na Ben Pol katika wimbo Pete.
Leo tunahamia kwenye vipengele vya Mtayarishaji wa wimbo Bora wa Mwaka kwa bendi, ambako Ababuu Mwana Zanzibar anachuana na Allan Mapigo na Amoroso na Mtayarishaji Chipukizi wa Mwaka, wanakochuana D Classic, Imma The Boy, Mensen Selecta, Mr T Touch na Sheddy Clever.
Watayarishaji wote waliongia fainali ni ambao kazi zao mwaka jana zilifanya vizuri katika medani ya muziki nchini kiasi cha kujipatia umaarufu mkubwa.
Hakika kuna ushindani mkubwa katika vipengele hivi na zaidi msanii atabebwa na idadi ya kura atakazopigiwa na mashabiki wake ili kushinda tuzo hiyo.
Wapiga kura wanatakiwa kuandika namba ya msanii, wimbo, kikundi au bendi anayotaka ishinde na kisha kutuma kwenda namba 15346, wakati njia nyingine zaidi ya ujumbe mfupi (SMS) ni pamoja na Email, kwenda ktma@innovex.co.tz au kutembelea tovuti ya www.kilitimetz.com na kupiga kura moja kwa moja.
Meneja wa Bia Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba, wamejiandaa vizuri mwaka huu kuhakikisha zoezi linafana.
Kilele cha sherehe za utoaji tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards zilizobeba kaulimbiu ya Kikwetu kwetu ni Juni 8, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, ambako pamoja na wasanii mbalimbali kupokea tuzo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pia.
Je, katika vipengele vya Mtayarishaji Bora wa Bendi wa Mwaka na Mtayarishaji Chipukizi, kura zako utawapa nani na nani?