IMEWEKWA MEI 21, 2013 SAA 8: 55 MCHANA
KLABU ya Liverpool ipo mbioni kumsajili beki wa kimataifa wa Ivory Coast, Kolo Toure kwa ajili ya msimu ujao.
Baada ya Jamie Carragher kustaafu na shaka iliyopo juu ya mustakabali wa Martin Skrtel na Sebastian Coates, kocha Brendan Rodgers anahitaji kutafuta angalau mabeki wengine wawili wa kati na hahitaji kupoteza muda kwa Toure.
Mkataba wa beki huyo wa zamani wa Arsenal katika klabu yake ya sasa, Manchester City unamalizika mwezi ujao na ameonyesha nia ya kubaki England na anaweza akawa mchezaji wa Liverpool kuanzia Julai 1, mwaka huu mara atakapofikia makubaliano na klabu hiyo.
Anakuja? Mkataba wa Kolo Toure Manchester City unaisha Juni
Rodgers amewatupia macho wachezaji kadhaa kuimarisha safu ya ulinzi ya Liverpool, wakiwemo Toby Alderweirled wa Ajax na Tiago Ilori wa Sporting Lisbon, lakini anamzimikia zaidi mchezaji wa kimataifa wa Ugiriki na klabu ya Schalke, Kyriakos Papadopoulos.
Chelsea pia inamuwania beki huyo mwenye umri wa miaka 21, lakini haiko tayari kuilipa Schalke Pauni Milioni 19 inazotaka ili kumuuza mchezaji huyo.
Ingawa Toure haendani na umri unaotakiwa na wamiliki wa Liverpool, Wamarekani, Fenway Sports Group – ana miaka 32, lakini inafahamika uzoefu unahitaji katika chumba cha kubadilishia nguo kufuatia kustaafu kwa Carragher.