Safari imeiva? Kocha Mfaransa Patrick Liewig |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 20, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
KOCHA Mfaransa wa Simba SC, Patrick Liewig anajiandaa kuondoka kurejea mapumzikoni nyumbani kwao, lakini hiyo inaweza kuwa safari yake ya moja kwa moja.
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka Simba SC, zinasema kwamba kocha tayari ametofautiana na viongozi kadhaa wa klabu hiyo na baadhi hazungumzi nao kabisa.
Inaonekana Mfaransa huyo naye amekwishajua anachungulia mlango wa kutokea na ameamua kutoondoka hadi alipwe malimbikizo ya mishahara yake ya miezi mitatu, Sh. Milioni 18.
Baada ya mechi ya juzi dhidi ya Yanga, inadaiwa kiongozi mmoja wa Simba SC alimfuata kocha huyo na kumshushia lawama kusababisha timu kufungwa 2-0 kutokana na upangaji wake wa kikosi.
Lakini Liewig anaonekana ni mtu asiyejali na aliye tayari kuondoka, ili mradi tu alipwe mafao yake.
Katika kipindi chake cha kuwa Simba SC tangu Januari mwaka huu, akimpokea Mserbia, Milovan Cirkovick, Liewig ameiongoza Simba SC katika mechi 25, akiiwezesha kushinda tisa, sare nane na kufungwa nane.
Kabla ya kutua Simba SC, Liewig amefundisha klabu kadhaa zikiwemo Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia.
Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa U20 na U18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na U16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990 alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Mitchel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998 alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso na kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.
Akiwa Simba SC msimu huu amefanya mapinduzi makubwa kikosini akiwaengua wakongwe na kuwapa nafasi wachezaji chipukizi, ambao kwa uzoefu waliokusanya wanaweza kuisaidia timu hiyo msimu ujao.