Anatakiwa: Stewart Hall akiwa kazini Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 23, 2013 SAA 12:10 ASUBUHI
BAADA ya kufanya vizuri akiwa na klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, Kocha Muingereza Stewart John Hall amegeuka lulu, sasa akiwa anatakiwa na klabu mbili za nchi tofauti na kwa dau kubwa.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Stewart alisema amepata ofa mbili zenye maslahi makubwa kuliko anayopata Azam FC kwa sasa, moja kutoka Libya na nyingine kutoka Canada.
“Lakini ofa nzuri zaidi ni ya Libya, ni fedha nyingi sana,”alisema Stewart.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu uamuzi wake, Stewart alisema kwamba tayari amezungumza na uongozi wa Azam FC juu ya hilo na umemuambia atulie kwani bado unamuhitaji.
“Sidhani kama nitakwenda, kwa sababu nimezungumza na uongozi wa Azam FC umesema bado unanihitaji. Nadhani nitabaki,”alisema.
Stewart Hall, alianza kuifundisha Azam FC mwaka 2011 na katika msimu wake huo wa kwanza, akaiwezesha timu kutwaa taji la kwanza, Kombe la Mapinduzi mbele ya vigogo Simba na Yanga kabla ya kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu mwishoni mwa msimu Mei, mwaka jana.
Julai mwaka jana aliiwezesha Azam FC kushika nafasi ya pili pia, katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame ikifungwa na Yanga SC 2-0 kwenye Fainali.
Baada ya hapo, akafukuzwa si kwa sababu ya uwezo, bali kukaidi agizo la uongozi, kutompanga mshambuliaji Mrisho Ngassa katika mechi hiyo, akaenda Sofapaka ya Kenya, nafasi yake akichukua Mserbia Boris Bunjak.
Lakini baada ya timu kuonekana imeshuka kiwango, alirejeshwa kazini Desemba mwaka jana na mwezi huo huo, akaiwezesha kutwaa Kombe la Hisani nchini DRC, kabla ya Januari kuiwezesha kutetea Kombe la Mapinduzi na mwezi huu kuiwezesha kushika tena nafasi ya pili katika Ligi Kuu.
Katika michuano ya Afrika, Azam ikishiriki kwa mara ya kwanza mwaka huu, Stewart aliiwezesha timu hiyo kucheza mechi tano bila kufungwa hata moja nyumbani na ugenini, kabla ya kufungwa 2-1 katika mechi ya sita ugenini, Rabat, Morocco na kutolewa katika Raundi ya Tatu Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat.
Tena siku hiyo, Azam ilipata penalti zikiwa zimebaki dakika nane mchezo kumalizika, ambayo kama John Bocco ‘Adebayor’ angefunga na kuwa sare ya 2-2, timu hiyo ingesonga mbele, lakini mkwaju wa mfungaji huyo bora wa zamani wa Ligi Kuu ukagonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani kabla ya kuokolewa.