Na Boniface Wambura, IMEWEKWA MEI 26, 2013 SAA 6:14 MCHANA
KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mdenmark Kim Poulsen amewatema wachezaji wawili, kipa Aishi Manula na Azam na mashambuliaji Juma Luizio wa Mtibwa Sugar katika kikosi kinachoondoka usiku wa leo kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuweka kambi ya mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kwenda Morocco.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya Shirika la Misri, ikiwa na kikosi cha wachezaji 21 chini ya Nahodha wake kipa Juma Kaseja.
Ameachwa; Kipa wa Azam, Aishi Manula ameachwa kikosi kinachokwenda Morocco |
Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.
Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa.
Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko.
Katika msafara huo wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Wakati huo huo: Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo ni mdhamini wa Taifa Stars, usikuwa jana ilikabidhi suti mpya 30 za kisasa kwa wachezaji wote na benchi la ufundi.
Suti hizo zilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa TFF Angetle Osiah na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa TBL, Phocus Lasway katika shughuli maalumu iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mpira. Shughuli hii pia ilitumiwa na Kilimanjaro Premium Lager kuiaga timu rasmi inapoondoka kwenda Ethiopia ili kujiandaa na mechi dhidi ya Morocco.
Wageni waalikwa walipata burudani ya aina yake pale ambapo wachezaji wenyewe pamoja na benchi zima la ufundi walipita mbele ya jukwaa kwa kujiamini ili kuonyesha suti mpya huku wakishangiliwa na pia watu waliokuwepo majumbani na sehemu nyingine walitoa maoni yao kwa njia ya twitter na facebook na maoni yao kuonyeshwa kupitia ‘scren’ kubwa zilizokuwepo ukumbini hapo.
Akizungumza katika tukio hilo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema wao kama wadhamini walipoanza kuidhamini Taifa Stars yapata mwaka mmoja sasa kwa kuwekeza zaidi ya bilioni 13 kwa miaka mitano, mojawapo ya jambo walilonuia kufanya ni kupandisha hadhi ya timu yetu na pia kuhakikisha ina mazingira mazuri ya kuleta ushindi.
Alisema suti hizo mpya zitawapa wachezaji wa Taifa Stars sura mpya kabisa kila wanaposafiri ndani na nje ya nchi kwani watafanana na wachezaji wengine wa kimataifa.
Alisema bali na suti hizo, wamefanya mambo mengine kama kukabidhi basi la kisasa kabisa la michezo ambalo limeiwezesha Taifa Stars kusafiri kwa raha kwani basi hilo lina uwezo wa kufanya safari hata za nchi jirani.
Aliwasihi wachezaji wajitume wanapoenda kuikabili Morocco katika mechi ya marudiano Mjini Marrakesh huku akisema Stars ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi hasa baada ya kuifunga Morocco 3-1 nyumbani.
“Ni matumaini yetu kuwa mutatupa raha zaidi kwa kuwafunga nyumbani kwao ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kufuzu,” alisema Kavishe na kuwasihi wajiandae vizuri pia na mechi ya Ivory Coast itakayopigwa Dar es Salaam Juni 16.
Kwa upande wake, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alitoa shukrani kwa Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwa mstari wa mbele kutekeleza mambo walioahidi kama wadhamini ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ari ya timu ya Taifa kufanya vizuri.
“Wametekeleza mambo waliyoahidi na kwa kweli hata wachezaji wanajiskia vizuri kuwa katika timu ta Taifa kwani wana uhakika wa kulipwa vizuri na kukaa sehemu nzuri wanapoingia kambini,” alisema.