Hoyce kushoto akiwapa darasa Miss Kigamboni |
Na Princess Asia, IMEWEKWA MEI 26, 2013 SAA 2:30 USIKU
MREMBO wa Tanzania mwaka 1999, Hoyce Temu, amewataka warembo hapa nchini kuwa na nidhamu na kutotumia mashindano hayo kama sehemu ya kujitafutia umaarufu.
Hoyce aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipotembelea kambi ya warembo wanaoshiriki wa shindano la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Redd's Miss Kigamboni 2013' litakalofanyika Ijumaa Juni 7 kwenye ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni.
Akizungumza na washiriki hao, Hoyce, aliwataka warembo kujiamini, kujiheshimu na kuwa mabalozi wema kwa jamii inayowazunguka hapa nchini kabla na baada ya kumaliza mashindano.
Hoyce aliwataka warembo hao kuwa na mawazo ya kujiendeleza na kamwe wasiridhike na elimu waliyonayo sana kwani urembo walionao hivi sasa una mwisho.
"Nawaomba mfahamu kuwa nyie ni madalali (mabalozi) wa jamii inayowazunguka na kila mara mfikiri kujiendelea, urembo sio kichaka cha wahalifu, wezi au kutumia miili yenu kufanya mambo yasiyokubalika na jamii," Hoyce alimaliza.
Naye mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya kinyang'anyiro hicho yanaendelea vizuri na kuongeza kwamba anaridhishwa na nidhamu na warembo.
Alisema kwamba kamati ya shindano hilo imejipanga kufanya shoo nzuri zaidi mwaka huu na kuwaambia wadau wa sanaa ya urembo kufika kushuhuria safari ya kumtoa mshindi wa taifa ikianzia kwenye kitongoji hicho.
Aliwataja warembo wanaoendelea na mazoezi kuwania taji hilo ni pamoja na Rogathe Michael, Irene Rajab, Magdalena Olotu, Latifa Mohammed, Axsaritha Vedastus, Angella Lutataza, Sara Makembo, Amina Mussa, Ellen Sulle, Rachel Reuben, Margareth Gerald na Zuhura Masoud.
Aliyataka makampuni na taasisi mbalimbali zinakaribishwa kudhamini shindano hilo ambalo mwaka jana lilitoa mshindi katika kinyang'anyiro cha Kanda ya Temeke ambaye ni Edda Sylivester.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu.
Wadhamini ambao wamethibitisha kusaidia shindano hilo ni pamoja na kampuni ya bia Tanzania kupitia kinywaji cha Redd's Premium Original,
Dodoma Wine, Montage Limited, Clouds Media Group, Papa Z, Logitik, Glolab Agency Limited, Cyn Henjewele na Wasemaje Blog.
Taji la Redd's Miss Tanzania linashikiliwa na Brigitte Alfred wakati Edda alishika alifanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye fainali hizo za taifa mwaka jana.