© Getty Images
Bosi mpya FIFA; Lydia amechaguliwa leo nchini Mauritius
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 31, 2013 SAA 11:15 ASUBUHI
RAIS mwanamke wa Chama cha Soka Burundi, Lydia Nsekera amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), akiweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza duniani kuingia ndani ya Kamati hiyo.
Lydia (46) anayetoka nchi moja na mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbangu alijipatia kura 95 na atakuwa madarakani kwa miaka minne, wakati Moya Dodd aliyepata kura 70 na Sonia Bien-Aime aliyepata kura 38, wataungana naye katika meza Kuu ya FIFA kama Wajumbe washirika waliochaguliwa naye kwa mwaka mmoja.
Hiyo inafuatia pendekezo lililotolewa na Rais wa FIFA, Sepp Blatter kuwa na Wajumbe zaidi wanawake. Mwanamama huyo wa Burundi, nchi jirani na Tanzania, Lydia Nsekera aliweka historia mwaka jana mjini Budapest katika Mkutano wa 62 wa FIFA alipochaguliwa kama Mjumbe Mshirika wa Kamati Kuu ya FIFA na kuweka rekodi pia ya kuwa mwanamke wa kwanza katika Kamati hiyo kwa mwaka mmoja.
Mkutano wa 63 wa FIFA nchini Mauritius uliojumuisha Wajumbe 209 ambao ni sawa na asilimia 99 umepiga hatua nyingine kubwa katika ushiriki wa wanawake ndani ya shirikisho hilo.
Nsekera ni Mjumbe wa 25 wa Kamati Kuu ya FIFA, ambayo ilikuwa ina Wajumbe 24 hadi leo. Uthibitisho wake wa kuwa Mjumbe wa FIFA katika Mkutano wa leo utamfanya awe madarakani kwa miaka minne.