Kimya kimya; Mwenyekiti wa kamati ya Usajili Simba SC, Zacharia Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 25, 2013 SAA 5:20 ASUBUHI
SIMBA SC usiku wa jana imesaini wachezaji watatu wapya kwa mpigo, akiwemo mshambuliaji hatari wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Zahor Iddi Pazi ambaye msimu uliopita alikuwa anatakiwa na Yanga SC akatimkia Azam FC.
Ametua Msimbazi; Zahor Pazi |
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameaimbia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mbali na Zahor anayechezea JKT Ruvu kwa mkopo akitokea Azam FC, wengine waliosajiliwa ni kipa Andrew Ntala kutoka Kagera Sugar na beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka Mtibwa Sugar.
Poppe, ambaye ni Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema wachezaji wote wamesaini mikataba ya miaka miwili kila mmoja.
“Bado tunaendelea na usajili wetu kwa umakini na kimya kimya. Nataka nirudie kusema kwamba, sera ya Simba SC si kusajili kutoka Yanga SC. Bali wao Yanga ndio wanasajili kwetu.
Nashangaa jana Katibu wao (Lawrence Mwalusako) ametamba ameniziba mimi mdomo baada ya kumsaini Haruna Niyonzima,”.
“Yule ni mchezaji wao, na sisi hatujawahi kutoa tamko la kumtaka yule mchezaji. Kama alikuwa anawatia presha ili wampe fedha nyingi kwa kuwahadaa Simba wanamtaka, amefanikiwa, ila sisi hakuwa kabisa katika mipango yetu,”alisema Poppe.
Poppe amesema Simba SC wanasajili kisayansi na si kama wapinzani wao hao, Yanga SC ambao wanaingia hasara ya fedha nyingi na wanacheza pata potea.
“Sisi tulimsajili Mbuyu Twite kama yeye tu, lakini wao wakaingilia akawapa sharti wamsajili na ndugu yake (Kabange Twite), wakaingia mkenge wakasajili mtu ambaye wamemlipa fedha nyingi, lakini hawajamtumia na hakuwa chaguo lao,”.
Kiboko ya Msuva; Issa Rashid 'Baba Ubaya' ametua Simba SC |
“Sasa sisi hatuna ulimbukeni wa aina ile katika kusajili, tunafanya mambo yetu kisayansi, na ndiyo maana wachezaji tunaosajili wanakuwa lulu na baadaye tunawauza nje kwa fedha nyingi tunapata faida kubwa, angalia Patrick Ochan, Emanuel Okwi na Mbwana Samatta. “Biashara nzuri sana. Hatukutumia hata Sh. Milioni 100 katika usajili wao, wameingiza karibu Milioni 700, Yanga wanaweza?”alihoji Poppe.
Poppe alisema pamoja na kusaini watatu hao wapya, Simba SC imewapa mikataba wachezaji wake kadhaa chipukizi waliopandishwa kutoka kikosi cha pili, akiwemo Haruna Chanongo ambaye alikuwa kwenye rada za Yanga pia.
Kusajiliwa kwa watatu hao wapya, kunafanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa Simba SC kufika wanne, baada ya Twaha Shekuwe ‘Messi’ wa Coastal Union kuwa mchezaji wa kwanza mpya kusajiliwa katika timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.
Lakini Simba SC, tayari imempoteza mchezaji mmoja, Mrisho Ngassa ambaye amesajiliwa na watani wa jadi, Yanga SC.