Ametua; Samuel Ssenkoomi amesaini miaka miwili Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 27, 2013 SAA 6:30 ASUBUHI
SIMBA SC imeendelea na harakati za ujenzi wa kikosi kipya hatari cha msimu ujao, baada ya saa mbili zilizopita kukamilisha usajil iwa beki wa kati wa kimataifa wa Uganda, Samuel Ssenkoomi anayechezea timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA).
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba Ssenkoomi amesaini mkataba wa miaka miwili kuchezea Wekundu hao wa Msimbazi.
Huyo anakuwa Mganda wa tatu katika kikosi cha Simba SC baada ya kipa, Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde na inawezekana hadi wiki ijayo, Wekundu hao wa Msimbazi wakatimiza idadi ya wachezaji wanne kutoka nchi hiyo, kwani hivi sasa wako mbioni kuinasa saini ya mshambuliaji hatari mno wa The Cranes.
Aidha, beki huyo mwenye nguvu na akili za mpira, anakuwa mchezaji wa tano mpya kusajiliwa Simba SC kwa ajili ya msimu ujao, baada ya awali kusajiliwa wachezaji wanne wazawa, kipa Andrew Ntalla kutoka Kagera Sugar, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka Mtibwa Sugar, kiungo Twaha Shekuwe ‘Messi’ kutoka Coastal Union na mshambuliaji Zahor Pazi kutoka Azam FC aliyekuwa anacheza kwa mkopo JKT Ruvu.
Simba SC imepania kuboresha kikosi chake ili kurejesha makali yake msimu ujao, baada ya msimu huu kutoka mikono mitupu, ikivuliwa ubingwa na kukosa hata nafasi ya pili, ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba SC ambayo mzunguko wa kwanza ilikuwa chini ya Mserbia, Milovan Cirkovick na mzunguko wa pili chini ya Mfaransa Patrick Liewig, imemaliza Ligi Kuu katika nafasi ya tatu nyuma ya Azam na Yanga mabingwa.
Kocha Mfaransa Patrick Liewig amepewa mishahara yake ya miezi miwili, Sh. Milioni 12 aliyokuwa anadai na tiketi ya kurejea kwao moja kwa moja na Abdallah Athumani Seif, maarufu ‘Kingi Kibadeni’, bila shaka atasaini mkataba wakati wowote kurithi mikoba.
Liewig sasa atakuwa anadai mshahara wa mwezi mmoja, Mei ambao uko ukingoni yeye akiwa tayari Ufaransa.
Simba SC pia imewaongezea mikataba wachezaji wake chipukizi kadhaa iliyowapandisha kutoka kikosi cha pili akiwemo Haruna Chanongo, ambaye alikuwa anapigiwa hesabu na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
Simba sasa inaelekeza nguvu zake katika usajili wa mshambuliaji sambamba na kusaini mikataba mipya na Nahodha wake Juma Kaseja pamoja na kiungo Amri Kiemba.