NYASI za Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mwakani hazitahimili vishindo vya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia kushuka kwa timu pekee ya Ligi Kuu kutoka jiji hilo kubwa, Toto Africans yenye maskani yake Mtaa wa Kishamapanda, katikati kabisa ya mji huo.
Toto imeaga Ligi Kuu, ikiwa imebakiza mechi moja kutimiza idadi ya michezo yake 26 ya msimu, kutokana na kuwa na pointi 22 na deni la mabao 12 zaidi ya kufungwa katika wastani wake wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mbali na Toto, timu nyingine ambazo zimekwishaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu ni African Lyon ya Dar es Salaam na Polisi ya Morogoro. Toto itatimiza pointi 25 ikishinda mechi yake ya mwisho na kufikia Mgambo JKT, lakini timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mbali na kuwa na mechi mbili zaidi, pia ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, imefungwa saba zaidi.
Maajabu gani yatokee Mgambo ifungwe mechi zote na Toto ishinde mabao si chini ya 8-0 katika mchezo wake mmoja tu ili ibaki Ligi Kuu? Ngumu, japo inawezekana.
Toto imekuwa moja kati ya timu sugu katika Ligi Kuu zilizozoea pilika za kupanda na kushuka na haitakuwa ajabu ikakosekana katika ligi hiyo kwa msimu mmoja tu ujao.
Ukitazama msimamo wa Ligi Kuu, utaona Toto ndiyo timu pekee iliyocheza mechi zaidi na imekuwa ikitangulizwa kwa wastani wa mechi mbili zaidi karibu mzunguko wote wa pili.
Na imekuwa hivyo wakati kwa muda mrefu msimu huu, mwendo wa Toto si mzuri katika Ligi Kuu. Vita ya timu kuepuka kushuka Daraja ilikuwa kubwa msimu huu na timu nyingi za Majeshi yetu ya ulinzi na usalama zilikuwa katika hali mbaya kwa pamoja na Toto na Lyon.
Mbali na Mgambo na Polisi, JKT Ruvu, JKT Oljoro na Prisons zote pia zilikuwa katika hali mbaya kabla ya baadaye baadhi kujinusuru. Dhahiri Ligi Kuu ilihitaji Ratiba yenye kwenda sambamba kwa timu zote, ili kukwepa uwezekano wa timu kupanga matokeo kwa kubebana.
Lakini Kamati ya Ligi Kuu haikuona umuhimu wa hilo- ikaacha Ligi iende bila mpangilio maalum na matokeo yake, Toto wamekuwa waathirika wa hilo. Nani ataisemea Toto timu fukara tu kutoka Kishamapanda ambayo haina hata uwezo wa kulipa mishahara wachezaji wake?
Na nani anajua umuhimu wa Toto katika soka yetu kwa ujumla- ikiwa timu ambayo inatambulisha vipaji vya Kanda ya Ziwa kwa ujumla, timu ambayo imetoa wachezaji wengi nyota katika soka ya nchi hii baada ya utawala wa Pamba FC ya mkoani Mwanza?
Lakini Toto kwa lolote au vyovyote, si kitu, ila kikubwa ni umuhimu wa Ligi ya haki na yenye muonekano wa haki, nani anajali? Sawa, Toto inashuka Daraja, lakini ukitazama mwenendo wa Ligi Kuu ulivyokuwa, huwezi kusema imeshuka, bali imeshushwa Daraja.
Nashangaa Toto wameendelea kukubali kuwa kivuli cha Yanga SC, wakati huwezi kuona inawasaidia vipi. Mchezaji mzuri wa Toto atakwenda Yanga kwa urahisi tu wakimtaka. Lakini mchezaji wa Yanga atakayekwenda Toto ni yule ambaye ameonekana hafai Jangwani.
Toto wanalia njaa msimu wote huu, hawana uwezo wa kujimudu na Yanga SC angalau wana hali nzuri, lakini wanawasaidiaje? Waswahili wanasema udugu kufaana bwana na si kufanana, si tu kwa sababu Toto na Yanga wanavaa rangi za aina moja, basi ni ndugu, hapana wanatakiwa kusaidiana pia.
Inafahamika Toto, ilianzishwa maalum kama tawi la Yanga SC pale Mwanza- lakini kwa ilipofikia, uongozi wa Yanga unatakiwa kutambua inahitaji msaada mkubwa ili kusimama imara.
Mwanza kuna matajiri wengi na makampuni mengi, lakini hayajitokezi kuisaidia Toto kwa sababu ni tawi la Yanga na huo ndio ukweli. Toto ni tawi la Yanga. Ajabu, Yanga wenyewe wanaisaidiaje hiyo Toto?
Umefika wakati sasa, lazima uongozi wa Yanga na Toto uketi meza moja pamoja na kujadili namna ya pande zote kunufaika na udugu huo, lakini pia kuimarisha udugu wenyewe- usiwe wa jina tu.