Fundi; Sure Boy akichezea mpira kwa ustadi wa hali ya juu viwanja vya Maamora, Rabat jana |
Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
MMOJA kati ya wanasoka wanaofanya vyema kwa sasa katika soka ya Tanzania, ni Salum Abubakar Salum, maarufu kam Sure Boy Jr., mtoto wa winga wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ aliyewika Yanga SC miaka ya 1980.
Kiungo huyo chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, anayeelekea kuufunika hata umaarufu wa baba yake katika soka, kwa sasa anachezea Azam FC na timu ya taifa, Taifa Stars, kote akiwa mchezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza.
BIN ZUBEIRY imefanya mahojiano na mchezaji huyo jana mjini Rabat, Morocco ambako yuko na Azam FC, ili kujua mengi kuhusu kiungo huyo, ikiwemo kufuata nyayo za baba yake, Yanga SC au la fuatlia mahojiano haya.
Mambo adimu; Unaweza kuona hadi mchezaji mwenzake Azam, Wandwi anamshangaa kwa nyuma mambo anayofanya Sure Boy |
BIN ZUBEIRY: Pole na uchovu wa safari kutoka Dar es Salaam hadi Rabat.
SURE BOY: Asante anko, tumekwishapoa kama hivi tunaendelea na maandalizi
BIN ZUBEIRY: Niambie, kwa sasa wakitajwa wachezaji bora 10 Tanzania, huwezi kukosekana kwenye orodha, unajisikiaje kwa hilo?
SURE BOY: Najisikia vizuri kwa kweli, naona kile ninachokifanya kinakubalika na wananchi
BIN ZUBEIRY: Unadhani nini si siri ya mafanikio yako?
SURE BOY: Nidhamu na kujituma, pia kuwa na ile kitu kiu ya kujifunza na kukubali kukosolewa, kushauriwa pia, yaani uwe unaambilika, usiwe mbishi, jeuri na mjuaji.
BIN ZUBEIRY: Baba yako ana mchango gani katika mafanikio yako?
SURE BOY: Aisee, mkubwa sana. Baba tena! Yeye ndiye kila kitu hadi mimi leo kuwa hivi. Kanizaa, kanilea, kanihudumia kila kitu wakati naanza, yaani mambo ya vifaa na nini, hadi nikasimama mwenyewe.
BIN ZUBEIRY: Ulitarajia siku moja utakuwa nyota mwenye jina katika soka kama baba yako?
SURE BOY: Hata baba ukimuuliza, niliwahi kumuambia, bwana wee usichoke kunihudumia masuala ya vifaa na nini, iko siku nitarudisha umaarufu wa jina lako katika soka ya bongo…wewe ukikutana naye muulize tu. Na ndiyo maana nikaamua kutumia jina la Sure Boy Jr. ili kuwakumbusha wapenzi wa soka wa nchi hii kuhusu mdingi wangu.
BIN ZUBEIRY: Na hapa ulipofika, nini matarajio yako zaidi?
SURE BOY: Hapa bwana katika safari yangu, mimi naona bado sana. Nia yangu haswa ni kucheza Ulaya. Na ninataka niondokee hapa hapa watu wanaona hivi hivi. Yaani uwezo wangu ndio unipeleke.
BIN ZUBEIRY: Uliingiaje, ukitokea wapi na lini Azam FC?
SURE BOY: Azam waliniona wakati nacheza timu yangu ya mtaani Friends Rangers mwaka 2007, wakanichukua tukapandisha timu na nimeendelea kuwa kwenye timu hadi sasa.
BIN ZUBEIRY: Ilikuchukua muda gani hadi kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza Azam?
SURE BOY: Yaani mimi tangu nachukuliwa Azam nacheza, sema tulipopanda msimu wa kwanza kwa sababu walisajiliwa wachezaji wakongwe nini kama akina Shaaban Kisiga na mimi nilikuwa bado mdogo sana, ikawa nasubiri subiri, lakini kwa sababu ya uwezo haikuchukua muda ikawa ile, panga pangua, Sure ndani.
BIN ZUBEIRY: Kwa msimu wa pili mfululizo, Azam mnashika nafasi ya pili Ligi Kuu, unazungumziaje mafanikio haya?
SURE BOY: Sisi tunafurahi, kwa sababu kwanza miaka mingi soka ya nchi hii imekuwa Simba na Yanga, lakini sasa hivi kuna Azam pia. Mwaka jana Yanga wamekaa benchi kwa sababu yetu na mwaka huu Simba pia wako benchi kwa sababu yetu, tunasikia raha kwa kweli.
BIN ZUBEIRY: Azam inahitaji muda gani zaidi ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu?
SURE BOY: Muda si mrefu, kwa mfano mwaka huu, sisi wenyewe kuna sehemu tulijichanganya, si unajua tena mambo ya mpira, lakini bila hivyo, Yanga wangekuwa nyuma yetu saa hizi. Ila poa, naamini msimu ujao ubingwa hautapotea njia tena.
BIN ZUBEIRY: Mnajiandaa kucheza na FAR Rabat mchezo wa marudiano Jumamosi, mkitakiwa kushinda au sare ya mabao, unadhani hilo litawezekana na ni ugenini?
SURE BOY: Tena sana. Sisi tunawatoa kabisa hawa Waarabu. Yaani sijui kitu gani tu, sisi tunapocheza Taifa, mechi zinakuwa ngumu, ila tukiwa ugenini tunacheza vizuri. Naamini kabisa tutafuzu kwa kuwafunga hawa jamaa hapa hapa kwao.
BIN ZUBEIRY: Unawazungumziaje wapinzani kwa ujumla?
SURE BOY: Si wazuri kihivyo, sema kwa sababu wanacheza kwao, watatusumbua kidogo. Najua dakika kama 15 za mwanzo watakuja sana kwetu, ila tukiweza kuhimili presha yao na kuwazuia wasipate bao kabla yetu, tutawang’oa.
BIN ZUBEIRY: Ni mchezaji gani Tanzania anayekuvutia zaidi na kwa sababu gani?
SURE BOY: Himid Mao. Huyu jamaa anajua, anajituma, ana nidhamu na hakati tamaa. Namkubali sana.
BIN ZUBEIRY: Kwa duniani?
SURE BOY: Cozorla (Santiago ‘Santi’ Cazorla Gonzalez)
BIN ZUBEIRY: Na timu gani unashabiki wewe Ulaya?
SURE BOY: Arsenal
BIN ZUBEIRY: Baba alicheza na kupata umaarufu mkubwa Yanga, ikiwemo jina la Sure Boy, watu watarajie siku moja utafuata nyayo zake pale Jangwani?
SURE BOY: Hiyo kama ngumu
BIN ZUBEIRY: Kwa nini?
SURE BOY: Kwa kucheza hadi kuwa mchezaji wa timu ya taifa na klabu kubwa kama Azam, tayari nimekwishafuata nyayo za baba.
BIN ZUBEIRY: Na Simba SC?
SURE BOY: Sidhani kama kuna kitu nakosa Azam. Sidhani kama Azam hawanikubali, ila sijui bwana, mambo ya mpira lolote linaweza kutokea.
BIN ZUBEIRY: Hadi sasa, soka imekusaidiaje katika maisha yako?
SURE BOY: Nina maisha yangu. Familia yangu inafurahia maisha. Nasaidia wazazi, namiliki mali zangu na nina ndoto za kupata zaidi. Basi.
BIN ZUBEIRY: Una mke na watoto wangapi sasa?
SURE BOY: Mke wangu Amina, ambaye Mungu katujaalia tumepata mtoto mmoja, tumemuita Abubakar, ana miaka miwili sasa.
BIN ZUBEIRY: Ungependa mwanao afuate nyayo zako kama wewe ulivofuata za baba?
SURE BOY: Yaani maji lazima yafuate mkondo. Kama mimi baba alivyonisaidia hadi kufika hapa, na mwanangu pia nitambeba hadi aweze kusimama mwenyewe.
BIN ZUBEIRY: Taifa Stars inaendelea vizuri chini yenu, Watanzania watarajie nini zaidi?
SURE BOY: Watarajie mambo makubwa tu. Tena makubwa sana. Kwa sababu tuna nia ya kuandika historia katika soka ya nchi hii.
BIN ZUBEIRY: Asante Sure, nikutakie maandalizi mema ya mechi na FAR Rabat.
SURE BOY: Asante anko. Kazi njema.
Sure Boy anaweza |
Sure Boy anajua |
Sure Boy mtalaamu |