Na Mahmoud Zubeiry
UHONDO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utahitimishwa kwa mchezo wa wapinzani wa jadi, Simba SC na Yanga Mei 18, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na hiyo ni kufuatia bingwa kuwa tayari amepatikana, Yanga SC na hata nafasi ya pili ni kama imekwishatulia kwenye himaya ya Azam FC.
Waliokuwa mabingwa watetezi msimu huu, Simba SC wanacheza kukamilisha ratiba na angalau kuhakikisha wanakuwa nyuma ya Yanga na Azam, ili kushika nafasi ya tatu.
Simba SC |
Ili mchezo wa watani Mei 18 uweo na mvuto, lazima Simba SC waonyeshe wanaweza kutoa upinzani kwa wapinzani wao hao wa kihistoria kwa kufanya vizuri katika mechi zake tatu kabla ya kucheza na Yanga.
Na mchezo wa kwanza kati hiyo mitatu kabla ya kukutana na mabingwa hao wapya, unafanyika leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Polisi ya Morogoro.
Kitakwimu na hesabu, Polisi wamekwishashuka Daraja, kwa sababu Mgambo JKT ya Tanga inaelekea kuwa na nafasi nzuri ya kubaki Ligi Kuu, lakini bado utakuwa mchezo mzuri tu wenye upinzani jioni ya leo.
Uzuri zaidi mchezo huu unakuja siku chache baada ya mgogoro uliokuwa unaendelea kwenye klabu ya Mtaa wa Msimbazi kumalizwa na sasa muungano umerejea Simba SC.
Kipenzi cha wapenzi wa Simba SC, Zacharia Hans Poppe aliyejiuzulu Machi 7, mwaka huu nafasi zake zote, Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na Uenyekiti wa Kamati ya Usajili amekubali kurejea madarakani, baada ya sharti lake la kutatuliwa kwanza kwa ugomvi uliokuwapo baina ya Mwenyekiti wa klabu, Alhaj Ismail Aden Rage na wapinzani wake kutekelezwa.
Na Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwa umoja uliopo sasa, wanataka kushinda mechi zote zilizobaki, mkazo zaidi ukiwa ni mpambano dhidi ya Yanga SC, ili wajenge heshima.
Poppe, amesema baada ya hapo wataelekeza nguvu zao kwenye kuunda kikosi imara cha msimu ujao, ambacho wanaamini kitarejesha ubingwa wa Ligi Kuu.
Bado haifahamiki, kama aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange 'Kaburu' aliyejiuzulu sambamba na Poppe, naye atarejea au la.
Baada ya leo, Simba SC watashuka tena dimbani Mei 5, kumenyana na Ruvu Shooting na Mei 8 na Mgambo JKT, mechi zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kutoka hapo, timu itavuka bahari kwenda Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga, Mei 18 ambao utafunga msimu huu wa Ligi Kuu.