MSHAMBULIAJI Mesut Ozil jana ameifungia mabao mawili Real Madrid katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Real Betis wakati vigogo hao wa Hispania wakijiandaa na Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alishirikiana vyema na Karim Benzema kuifungia Madrid bao la kwanza karibu na mapumziko, kabla ya Mfaransa huyo kumalizia shambulizi la kushitukiza dakika ya 57 kwa pasi Cristiano Ronaldo kufunga la pili.
Ozil akafunga tena dakika ya mwisho kabisa wakati Betis ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Jorge Molina aliyetokea benchi kwa penalti dakika ya 72, kufuatia Nacho Fernandez kumchezea rafu Ruben Castro katika eneo la hatari.
Anafunga la pili: Mesut Ozil alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 wa Real Madrid dhidi ya Real Betis
Mashabiki walikaa kimya kwa dakika moja kabla ya mchezo kuanza kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kuwaenzi waathirika mlipuko wa mabomu kwenye mbio za Boston Marathon.
Kocha wa Madrid, Jose Mourinho aliwapumzisha wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza wakiwemo mabeki na kiungo na mkajabi.
Kiungo Mbrazil, Casemiro aliichezea Real Madrid mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na na kikosi chao cha wachezaji wa akiba akitokea Sao Paulo msimu huu, wakati kinda Fernandez alianza katika beki ya kulia.