Said katikati akiwa na Barthez kulia na kocha wa makipa wa Yanga, Razack Ssiwa kushoto |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA Said Mohamed Kasarama wa Yanga, amesema anashukuru ametoa mkosi jana kwa kwa kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Said aliingia dakika ya 86 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana kumpokea Ally Mustafa ‘Barthez’ aliyeumia kiuno Yanga SC ikimenyana na JKT Ruvu na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Katika dakika takriban 10 alizodaka zikiwemo za majeruhi, Said alicheza krosi moja tu ambayo ilionekana kuwa ya hatari na ‘kupata’ zawadi ya makofi ya mashabiki wa timu yake, ambao walionekana kuwa na wasiwasi naye wakati anaingia.
“Da! Nashukuru nimetoa mkosi mwanangu,” alisema Said wakati akizungumza na Geoffrey Taita ambaye jana hakuvaa kabisa jezi wakati akirejea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mechi hiyo.
Ametoa mkosi; Said Mohamed Kasarama amedaka mechi ya kwanza jana Yanga SC msimu huu |
Msimu uliopita Said alikuwa kipa namba mbili Yanga baada ya Yaw Berko wa Ghana, lakini katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, alikuwa kipa wa tatu, baada ya Berko na Barthez.
Lakini kuachwa kwa Berko mzunguko wa pili, kumemrudisha katika nafasi ya kipa wa pili, ingawa jana ndiyo alidaka kwa mara ya kwanza msimu huu.
Said aliye katika msimu wa pili Yanga SC tangu asajiliwe kutoka Majimaji ya Songea mkoani Ruvuma, alitua Jangwani akiwa kipa wa timu ya taifa, Taifa Stars lakini benchi limemfanya asiendelee kuitwa kikosini.
Ushindi wa Yanga jana unawafanya watimize pointi 56 na sasa wanahitaji pointi tatu zaidi katika mchezo wao ujao dhidi ya Coastal Union ya Tanga ili rasmi kubeba ubingwa, ulioachwa wazi na waliokuwa watetezi, Simba SC.
Ila wanaweza kusherehekea ubingwa nje ya Uwanja, iwapo Azam FC watafungwa na Coastal Ijumaa Tanga.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Orden Mbaga, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Simon Msuva, ambaye alifunga kwa ustadi wa hali ya juu.
Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Mbuyu Twite ambaye alimrushia mfungaji akawahadaa mabeki wa JKT Ruvu na kuingia kwenye ‘sita’ akifanya kama anataka kutoa pasi, lakini akafumua shuti kali moja kwa moja kufunga.
Hata hivyo, baada ya bao hilo, wachezaji wa JKT Ruvu walimfuata mshika kibendera namba mbili, Lulu Mushi wakilalamikia bao hilo, wakidai lilitokana na maamuzi yasiyo ya haki ya mdada huyo.
Walilalamika mpira waliopewa Yanga warushe walistahili kurusha wao, JKT kwani aliyeutoa ni mshambuliaji wa Yanga, Hamisi Kiiza.
Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi na moto zaidi na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi, yaliyofungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 59 na Nizar Khalfan dakika ya 64.
Kiiza alifunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na David Luhende, baada ya Nizar Khalfan kuchezewa rafu nje kidogo ya eneo la hatari.
Nizar yeye alifunga baada ya kuuwahi mpira uliogonga mwamba na kurudi baada ya Frank Domayo kuunganisha krosi ya Haruna Niyonzima.