Kenny Mwaisabula; Ataiua Yanga SC leo? |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA wa zamani wa Yanga SC, Kenny Mwaisabula amerithi mikoba ya Charles Kilinda aliyefukuzwa wiki tatu zilizopita katika timu ya JKT Ruvu ya Pwani, iliyohamishia maskani yake Dar es Salaam kutokana na matokeo mabaya.
Na mtihani wake wa kwanza ‘King Kenny’ ni jioni hii akiiongoza timu hiyo ya Jeshi dhidi ya timu yake hiyo ya zamani, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Katika mchezo huo unaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:15, Yanga inahitaji ushindi ili kujisogeza karibu na ubingwa, wakati JKT inahitaji pointi tatu ili kujiondoa kwenye hatari ya kushuka Daraja.
Unatarajiwa kuwa mchezo mkali na wa kusisimua kutokana na ukweli pia, wachezaji wa JKT hupenda kucheza kwa kukamia kwenye mechi dhidi ya timu kubwa, Simba, Yanga na Azam FC.
Na kwa muda mrefu tangu amekuwa nje ya kazi, Mwaisabula amekuwa mchambuzi ambaye amekuwa akikosoa sana mbinu za makocha wa timu kubwa pamoja na timu ya taifa, hivyo leo naye atamulikwa akiiongoza JKT dhidi ya Yanga.
Tayari vikosi vya mechi ya leo vimekwishatoka na Mwaisabula ameipangia kikosi hatari Yanga SC ambacho ni; Shaaban Dihile, Hassan Kikutwa, Stanley Nkomola, Ramadhani Madenge, Damas Makwaya, Nashon Naftali, Amos Mgisa, Ally Mkanga, Mussa Mgosi, Zahor Pazi na Haroun Adolph.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Hamisi Kiiza na Simon Msuva.