Wachezaji wa Yanga wanatimka kushangilia- angalia viatu vingapi vyekundu hapo? |
Na Mahmoud Zubeiry
MOJA kati ya vitu ambavyo vinanogesha upinzani wa jadi wa Simba SC na Yanga SC ni rangi zao. Na unawezaje kutambua upinzani wa timu hizo kama si kwa rangi zao, Simba SC nyekundu na nyeupe na Yanga SC kijani na njano.
Inaweza kutokea bahati mbaya, Yanga SC wakakutwa na rangi nyeupe kwenye sehemu ya vifaa vyao vya michezo kwa ujumla- lakini si nyekundu.
Hiyo wanaita haramu. Imetokea bahati mbaya kidogo, basi kubwa walilopewa Yanga SC na wadhamini wao, TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) kwenye nembo ya bia Kilimanjaro kuna rangi nyekundu. Pale walikosa ujanja wakapokea.
Lakini jezi, iwe na rangi nyekundu. Hawapokei. Walikuwa tayari kuingia katika mgogoro na wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom kwa ajili ya nembo yenye rangi nyekundu katika jezi zao. Vodacom ilibidi wawabadilishie jezi.
Kwa Simba SC nako, wao ndio hakuna rangi hata moja iwe kijani au njano wanaitaka katika jezi zao. Haramu kabisa.
Na mashabiki wa timu hizo, hawapendi hata kuwaona wachezaji wao wakiwa na punje ya rangi za wapinzani kwenye vifaa vyao vya michezo, haswa wakati wa mechi.
Ila, kuna baadhi ya wachezaji wa timu hizo wamekuwa vichwa ngumu- wanavaa viatu vya rangi za wapinzani. Huko jukwaani, huwa wanalaani si kidogo mchezaji anayefanya hivyo.
Shomary Kapombe wa Simba amevaa viatu vya njano |
Mwinyi Kazimoto wa Simba SC amevaa viatu vya njano |
Hamisi Kiiza wa Yanga kushoto anapiga shuti kwa kiatu chekundu |
Simon Msuva kushoto na Athumani Iddi 'Chuji' wa Yanga SC, walikosa viatu vingine maduka yote wakanunua hivi? |
Itokeee bahati mbaya au nzuri ni mchezaji nyota na tegemeo la timu watameza fundo za mate, kutuliza maumivu ya moyo, lakini watazungumza maneno mabaya dhidi yake.
Ushabiki wa Simba na Yanga ni wa aina yake- katika suala la rangi hakuna mzaha na imeshuhudiwa mara kadhaa mtu anayekatiza kwenye eneo la wapinzani akiwa amevaa rangi za wapinzani anapewa mkong’oto wa kufa mtu.
Na hata askari hawawezi kukusaidia, watakuuliza; “We hukusoma mlangoni unaingia choo gani kabla ya kuingia? Umekosea mwenyewe, pole jifunze siku nyingine usirudie kosa, watakuua”.
Ajabu, kwa mashabiki wengi wa Yanga SC, wanachukia rangi nyekundu hapa, lakini timu zao nyingi wanazoshabiki England ni zile zinazovaa jezi nyekundu.
Waungwana, nitakuwa nimekosea nikisema Yanga SC wengi ni Manchester United, ambao tena wanaitwa Mashetani Wekundu? Na hao mashabiki wa Yanga wanavaa jezi za Manchester, tena zile nyekundu kabisa- ingawa hawawezi kuthubutu kuja nazo uwanjani timu yao ikicheza.
Simon Msuva na viatu vya rangi haramu Yanga SC |
Mwinyi Kazimoto na viatu haramu kabisa Simba SC |
Said Mohamed wa Yanga viatu vyake vina rangi nyekundu |
Shomary Kapombe ni kipenzi cha mashabiki wa Simba SC, lakini kwa viatu hivi... |
Timu nyingi zinazovaa jezi za kijani na njano England ni zile ndogo ndogo ambazo hazina mashabiki hapa nyumbani, lakini najua wapo Simba ni mashabiki wa Swansea City. Vipi hao nao?
Ndiyo hao hao Yanga wa Man U na Simba wa Swansea City wanaowatukania mama zao wachezaji kwa kuvaa viatu vya rangi nyekundu. Usimba na Uyanga kaazi kweli kweli- na kama wachezaji wanaaovaa viatu vyekundu wangejua wanavyotukaniziwa majukwaani, wangeacha tu. Chachandu kidogo wakati mwingine. Ipokeeni wapendwa.