NIPO Morocco tangu Jumatatu na kikosi cha Azam FC, ambacho kimekuja kucheza na wenyeji AS FAR Rabat katika mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho Afrika Raundi ya Tatu. Namshukuru Mungu, kwa mara nyingine nimefika katika nchi iliyopiga hatua ya kimaendeleo katika sekta ya kimichezo, siyo soka tu.
Hii ndiyo nchi ambayo anatokea bondia Abdelhak Achik, mshindi wa Medali ya Shaba uzito wa Feather katika mashindano ya Olimpiki mwaka 1988 mjini Seoul. Ndugu yake, Mohamed Abdelhak Achik pia alishinda Medali kama hiyo katika Olimpiki ya mwaka 1992 mjini Barcelona.
Sahau kuhusu wanasoka wote maarufu unaowajua wanaocheza, waliocheza Ulaya walitokea, wanatokea Morocco, akiwemo Mwanasoka Bora wa zamani wa Afrika Mustafa Hadji- elewa hata Yossi Benayoun, Muisrael anayechezea Chelsea wazazi wake wanatokea Morocco. Cyril Abidi, bingwa wa mchezo wa Muay Thai (jamii ya Kick Boxing) duniani, anatokea Morocco.
Hii ndiyo nchi anayotokea mmoja wa warembo maarufu wanaocheza mieleka WWE, Layla El ambaye pia ni dansa, mwanamitindo na mwigizaji. Hii ni nchi ambayo anatokea Said Aouita, mwanariadha maarufu duniani aliyeweka rekodi duniani. Mbali na kushinda mbio za mita 5000 katika Olimpiki ya 1984 na mashindano ya dunia mwaka 1987, pia amewahi kuweka rejkodi za dunia katia mbio za mita 1500 (dakika 3:29.45), mita 2000 (dakika 4:50.80), mita 3000 (dakika 7:29.46), na mara mbili mita 5000 (dakika 13:00.40 na dakika 12:58.39).
Sijui nielezee vipi Morocco, ina mashujaa wengi katika michezo- labda niongeze kwamba hii ni nchi ambayo imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, mara mbili kupitia kwa Raja Casablanca 1997 na 1989 na mara moja moja kupitia kwa Wydad Casablanca 1992 na FAR Rabat 1985. Imetwaa mataji matatu ya Kombe la Shirikisho, FAR Rabat (2005), FUS Rabat (2010) na MAS Fez (2011).
Timu ya taifa ya Morocco imecheza Kombe la Dunia tumewahi kuiona kupitia Luninga zetu nyumbani Tanzania- na ni mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1996. Kwa ushindani uliopo miongoni mataifa imara katika soka barani, haya si mafanikio haba kwao. Angalau.
Na sikushangaa baada ya kufika hapa kwa nini Morocco ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye mafanikio katika michezo, kwani nimejionea uwekezaji mkubwa na thamani ya hali ya juu wanayopewa wanamichezo wa hapa, wakiwemo wale wadogo kabisa wanaoanza katia hatua ya awali.
Narudi nyumbani, tunalalamika, tunalia hatufanyi vizuri katika michezo, lakini kuna uwekezaji gani pale nyumbani? Ikitokea wanamichezo wetu wakafanya vizuri kwa bahati zao au juhudi zao binafasi, basi wenye nchi wataibuka, watasema mengi, wataahidi mengi, watakumbusha mengi- mwisho wa siku hakuna lolote.
Na mbaya zaidi, wanamichezo wa Tanzania hawathaminiwi kabisa, Serikali haijui hawa watu walicheza kwa Ridhaa katika wakati ambao mwamko ulikuwa mdogo sana na hawakupata kitu zaidi ya sifa na kuitwa mashujaa, ambao wengi wao wamekufa masikini, walio hai wapo kwenye dimbwi la ufukara, wanateseka na maradhi na kila aina ya kadhia.
Lini Mohamed Chuma alienziwa Tanzania tangu kifo chake au Omar Mahadhi na Maulid Dilunga, wachezaji wa kombaini ya Afrika mwaka 1973? Hakuna. Hii ndiyo Tanzania bwana.
Nataka nikumbushe kitu kimoja, Novemba mwaka 2010, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alilihutubia Bunge na kusema kwamba, michezo ni miongoni mwa vipaumbele vyake katika ngwe ya mwisho ya utawala wake.
Kwa sababu hiyo, Kikwete akatoa tahadhari kwamba umefika wakati sasa wa kuimarisha uongozi na utendaji wa klabu pamoja na vyama vya michezo, badala ya kugombania uongozi na maslahi binafsi.
Alisema hali hiyo itasaidia muda mwingi kutumika kuendeleza vipaji vya wanamichezo hapa nchini, badala ya hali ilivyo sasa, ambapo muda mwingi hutumika kugombania uongozi na maslahi binafsi.
Rais Kikwete, anayemalizia miaka yake mitano madarakani, alisema kuwa katika miaka mitano iliyopita, Serikali ilijitahidi kuweka mazingira mazuri kwenye michezo na kusaidia kuwapa vijana ajira. Alisema migogoro huwa inamkera, mambo ya kugombana na kufukuzana kwenye uongozi hayana tija na sasa wayaweke pembeni.
Alisema alitimiza ahadi yake ya kugharimia makocha wa kigeni wa michezo mbalimbali watakaochaguliwa na vyama vya michezo husika na kwamba hivi sasa makocha wa mpira wa miguu, ndondi, riadha na netiboli kutoka nchi tofauti wapo nchini.
Hata hivyo, Kikwete alisikitika bado nchi haijapata mafanikio ya juu, ingawa alikiri mwanga wa matumaini unaonekana na kusisitiza kinachotakiwa sasa ni kuimarisha uongozi na utendaji wa vyama na vilabu vya michezo husika, ili muda mwingi utumike kuendeleza vipaji vya wanamichezo wetu badala ya hali ilivyo sasa ambapo muda mwingi hutumika kugombania uongozi na maslahi binafsi.
Rais alisema katika kipindi hicho, serikali yake imerejesha michezo shuleni na kwamba inahitajika kujipanga zaidi kufanikisha michezo mashuleni kwa kufundisha walimu wa michezo na kuhakikisha viwanja na vifaa vya michezo vinapatikana shuleni.
Alisema wakati umefika kwa vyama au vilabu vya michezo kuanzisha shule za michezo yao, ili kukuza vipaji vya vijana mapema. Pamoja na hayo, Rais pia alipongeza kukua kwa sanaa za maonyesho ambazo ni muziki na filamu na kumeibuka wanamuziki wengi wazuri wa kizazi kipya, taarabu na rumba, akimtaja Mzee Yussuf aliyetumbuiza kwenye harusi ya mwanawe, Ridhiwani wakati anao kama mfano.
Hakusitia pia kupongeza maendeleo makubwa ya filamu na uigizaji na kuwapa matumaini wasanii kwamba kuna haja ya kujipanga vizuri kusaidia kuendeleza sanaa hizo na wasanii wake na kwamba yeye binafsi ameanza kuchukua hatua za hapa na pale za kujaribu kutatua baadhi ya matatizo yanayowakabili.
Akasema, wakati umefika sasa kuwa na mipango thabiti ya kuendeleza fani hizo na kuwawezesha wasanii kuendeleza vipaji vyao na kunufaika na kazi zao. Naamini, wapenda michezo wengi waliipokea kwa faraja kubwa hotuba hiyo ya Rais Kikwete na kuamini kwamba wakati wa kufurahia matokeo mazuri katika michezo umekaribia.
Lakini kimsingi kwa kurejea utawala wa awamu iliyotangulia, chini ya BM (Benjamin Mkapa)- alipokuwa katika miaka yake mitano ya mwisho alitoa ahadi ya kuwaachia zawadi nzuri wapenda michezo- nayo si nyingine zaidi ya Uwanja wa kisasa, wengi wanaamini JK atafanya.
Na wanasubiri kwa hamu kuona, atafanya nini, ili akiondoka wamkumbuke kwa zawadi atakayowaachia wapenzi wa michezo nchini. Hali halisi katika sekta ya michezo Tanzania hivi sasa ni mbaya, inatia kichefuchefu.
Michezo hiyo kwa sasa ni yatima, haina msaada, wafadhili hawajitokeza kuisaidia. Wamejikita zaidi kwenye soka, lakini tukirejea nyuma iliitangaza vizuri nchi yetu katika medani ya kimataifa.
Majina kama Habib Kinyogoli ‘Master’, Emanuel Mlundwa, Titus Simba (marehemu), Lucas Msomba, Nassor Michael, Michael Yombayomba- yaliitangaza vema nchi yetu katika michuano mikubwa ya ndondi, wakati kwenye Riadha watu kama Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Gidamas Shahanga, Francis Naali na wengine yalitangaza vema nchi yetu katika medani ya kimataifa.
Lakini kwa sasa huwezi na kuwa na matumaini ya kupata mashujaa kama hao, kwa sababu hali ni ngumu, michezo hiyo haina sapoti, haina wafadhili. Wewe kambi ya timu ya taifa bondia anaambiwa aende kwa nauli yake, vifaa vya michezo ajinunulie.
Bado magwiji wa michezo hii wanajitolea mno kuzalisha vipaji vipya pamoja na hali hiyo ngumu, wanafanya kwa mapenzi yao. JK amtembelee Kinyogoli pale Amana, ajionee kazi anayoifanya ya kufundisha ngumi kuanzia watoto na anapata wapi sapoti. Shahanga naye ana kituo cha kuzalisha vipaji, lakini analia hajapata sapoti.
Ilikuwa Novemba mwaka 2010 wakati rais JK anatoa ahadi hiyo ya kuwekeza kwenye michezo katika miaka mitano ya mwisho, ambayo sasa tupo katika mwaka wa tatu. Naamini, wapenda michezo bado wanakumbuka ahadi hiyo na wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wake.
Nakumbuka na nilikuwepo kwenye mapokezi ya bondia Michael Yombayomba akirejea na Medali ya Dhahabu ya ndondi za Madola uzito wa bantam, pia kwenye mapokezi ya Naali akirejea na Medali ya Dhahabu ya Riadha ya Madola pia. Mapokezi ya Rashid Matumla akirejea ubingwa wa Dunia uzito wa Light-middle baada ya kumpiga Paolo Pizzamigilio kwao Italia.
Maelfu walishiriki mapokezi hayo na kuandama kuanzia Uwanja wa Ndege hadi mjini wakishangilia ushindi huo. Naamini wana hamu ya kujumuika tena na tena pamoja kushangilia mashujaa wa taifa leo. Lakini watatoka wapi mashujaa hao ikiwa hali ni mbaya kwenye michezo? JK anapaswa kujua, Watanzania wanakumbuka ahadi yake. Hizi ndizo salamu zangu kwake na kwa Watanzania wote kutoka hapa Rabat, Morocco Jumatano ya leo. Wasalaam.