Ametoa onyo; Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema Kapombe haondoki Msimbazi |
Na Prince Akbar
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amewaasa Azam FC na Yanga SC waache kumfuatafuata mchezaji wao Shomary Kapombe, kwani ana mkataba na hana mpango wa kuhama Msimbazi.
“Sisi tunajua, hawa watu wanamfuatafuata sana huyu mchezaji na amekuwa akituambia, tunaomba wamuache, watajisumbua bure na sana waishie kuliwa fedha zao bure,”alisema Poppe.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi lwa Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba Simba SC inamuandalia maisha mazuri ya soka Kapombe, ambayo klabu nyingine yoyote nchini haiwezi.
Haondoki; Shomary Kapombe atakwenda Sunderland |
“Mchezaji yeyote mwenye kutaka mafanikio lazima atayatafutia Simba SC, kwa sababu tuna historia hiyo. Tumetoa wachezaji wengi tu kwenda Ulaya tangu enzi za akina Nico Njohole, mdogo wake Renatus. Kwa ujumla, wachezaji ambao wanakwenda kucheza njia kwa mafanikio, wanatokea Simba SC,”alisema.
Akitoa mifano zaidi, Hans Poppe alisema Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya DRC, Danny Mrwanda aliye Vietnam, Henry Joseph anayecheza Norway wote wametoka Simba SC.
“Na si hao tu, hata wachezaji wa kigeni wanaokuja hapa, wamekuwa wakipatia maisha hapa Simba SC, mfano akina William Fahnbullar (Liberia), Emeh Izhuchukwu (Nigeria), Patrick Ochan na Emanuel Okwi (Uganda),”alisema.
Poppe amesema Kapombe atahamia Ulaya muda si mrefu; “Kila mtu anajua, huyu kijana anatakiwa Sunderland na wamekuwa wakimfuatilia sana. Sasa Azam au Yanga wasijidanganye eti huyu mchezaji atababaikia ofa zao, aache msiah mazuri Ulaya,”alisema.