WAWAKILISHI pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya Afrika, Azam FC jana wamelazimishwa sare ya bila kufungana na AS FAR Rabat ya Morocco katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Tatu, Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo kidogo yanaonekana kuwakatisha tamaa baadhi ya wapenzi na wadau wa soka nchini, wanaamini huo ndiyo mwisho wa safari ya Azam kwenye michuano hiyo. Wanadhani ni yale yale, ya vigogo wa soka nchini Simba na Yanga, vinapokutana na timu za Kaskazini mwa Afrika- kwa asilimia kubwa hazifurukuti.
Kweli si matokeo ya kufurahisha kwa nyumbani, kwani sasa Azam imejiwekea mtihani mgumu katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo Morocco, wakitakiwa lazima kushinda au kutoa sare ya mabao ili kufuzu.
Nilikuwapo Uwanja wa Taifa jana, pamoja na sare hiyo, Azam walicheza soka maridadi na ya ushindani kiasi cha kukaribia kufunga si chini ya mara tatu majaribio mazuri zaidi yakitoka kwa washambuliaji wao wa pembeni, Kipre Herman Tchetche mara mbili na Khamis Mcha ‘Vialli’ mara moja,
Kipre aligongesha mwamba mashuti mawili katika dakika za 51 pembeni kushoto katikati na dakika ya 90+1 mwamba wa juu katikati baada ya jitihada za kuwatoka mabeki wa AS FAR Rabat.
Khamis Mcha naye alimtoka vizuri beki wa pembeni wa AS FAR Rabat dakika ya 52 lakini akapiga nje shuti lake.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emile Fred wa Shelisheli, aliyesaidiwa na nduguze Steve Maire na Jean Ernesta pembeni, kipindi cha kwanza Azam walionekana kucheza kwa tahadhari zaidi na kufanya mashambulizi machache.
Bahati mbaya zaidi, Azam walipata pigo kubwa dakika ya saba tu ya mchezo huo, baada ya beki wake Mkenya, Joackins Atudo kuumia na kushindwa kuendelea kucheza, nafasi yake ikichukuliwa na Luckson Kakolaki.
Binafsi ile ilinirusha roho kidogo, kuumia kwa Atudo hadi kutoka, beki ambaye tangu ameanza kucheza mechi ya kwanza Azam aliposajiliwa Desemba mwaka jana hajakosa mechi nyingine yeyote- amekuwa roho ya safu ya ulinzi ya timu na mbaya zaidi anayeingia ni Kakolaki, yule ambaye alikuwa uchochoro wa Mrisho Ngassa katika mechi iliyopita ya timu hiyo dhidi ya Simba SC!
Lakini ‘Mungu saidia’, Kakolaki alipoingia alikwenda kucheza vizuri mno na kwa utulivu wa hali ya juu, hivyo kufanya safu ya ulinzi ya Azam iendelee kuwa imara.
Tuliona kipindi cha pili, Azam walivyobadilika na kufunguka, wakianza kushambulia moja kwa moja kwa pasi ndefu jambo ambalo liliweka kwenye misukosuko lango la AS FAR Rabat kwa muda mrefu hadi wachezaji wa timu hiyo kuanza kufanya hila za kupoteza muda ili kupunguza kasi ya wenyeji.
Tuliona namna ambavyo John Raphael Bocco ‘Adebayor’ naye alilitia misukosuko mara kadhaa lango la wageni kila ilipoingizwa mipira ya juu kutokea pembeni hususan kona japokuwa alikuwa chini ya ulinzi mkali jana.
Wachezaji wa pembeni, Kipre na Mcha walikuwa mwiba mno kwa safu ya ulinzi ya FAR Rabat, timu ya jeshi la Morocco, wakati huo huo, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alitawala vyema sehemu ya kiungo tofauti na kipindi cha kwanza.
Pale chini, Kipre Balou alifanya kazi yake vizuri- mabeki wa pembeni Himi Mao na Waziri Salum walikuwa wakikaba na kusaidia mashambulizi vizuri tu. Azam ilicheza vizuri sana kipindi cha pili na kilishoshindikana ni mpira tu kuingia nyavuni.
Pamoja na hofu ya baadhi ya wapenzi wa soka, kwamba Azam huenda ikawa imefikia mwisho wa safari yake katika michuano hii, lakini naweza kutofautiana nao, tena kwa sababu mbili tu kubwa.
Kwanza ni kiwango cha mchezo wa jana, tumeona Azam ilikuwa bora uwanjani kuliko wapinzani wao na pili, matokeo mabaya Uwanja wa Taifa, yanaonekana sasa kuwa ya kawaida kwa wawakilishi wetu hao, lakini wanakuwa wakali mno wanapocheza ugenini.
Katika Raundi ya Kwanza, Azam walibanwa mno Taifa na wapinzani wao Al Nasir Juba na ilibaki kidogo mchezo uishe kwa sare ya 1-1 kama si mabao ya dakika za lala salama ya Kipre, lakini mchezo wa marudiano ugenini walishinda 5-0 hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 8-1.
Katika Raundi ya Pili, Azam baada ya kushinda 2-1 ugenini, walikuja katika mchezo mgumu sana Dar es Salaam dhidi ya Barack Young Controllers II ya Liberia na ilionekana kama wapinzani wangeweza kupata bao 1-0 walilohitaji na kuitoa timu ya Tanzania, lakini shukrani dakika 90 ziliisha 0-0.
Sijui kuna nini kinawafanya wachezaji wa Azam wanashindwa kuumudu Uwanja wa Taifa, lakini imani inabaki pale pale, wanakuwa hatari sana wanapocheza ugenini na hilo ndilo ninalolitarajia katika mchezo wa marudiano dhidi ya FAR Rabat wiki mbili zijazo.
Na vizuri zaidi ni kwamba mchezo wa kwanza hakukuwa na bao, wapinzani japo watakuwa nyumbani, lakini watakuwa kwenye wakati mgumu zaidi kwa sababu hata sare ya mabao watang’oka wao. Kufikiria sare kwa soka ile iliyochezwa na Azam jana ni mbali sana, kuna matumaini makubwa Azam kushinda ugenini.
Kila la heri kwa wawakilishi wetu hao. Mungu ibariki Azam, ibariki Tanzania. Amin.