Wachezaji wa Azam baada ya kutua Dubai, wakisubiri kugongewa viza kuingia nchini humo usiku huu |
Na Mahmoud Zubeiry, Dubai
AZAM FC imewasili salama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai usiku saa 6:00 kwa saa za hapa sawa na saa 5:00 kwa saa za Afrika Mashariki, ikitokea Dar es Salaam ikiwa njiani kuelekea Morocco kumenyana na wenyeji, FAR Rabat katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Tatu Kombe la Shirikisho Afrika.
Msafara wa huo unaouhusisha wachezaji na benchi la Ufundi, baada ya awali viongozi na wapenzi kadhaa kutangulia nchini humo, ili kuweka mazingira sawa, uliondoka Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la Emirates, wadhamini wa Arsenal ya England saa 11:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Ni safari ndefu inayohusisha mabara mawili, kutoka Afrika, Tanzania kupitia Asia Dubai na kurudi Afrika nchini Morocco.
Azam watalala katika hoteli ya nyota tano ya Copthorne kabla ya kuunganisha ndege saa 7:35 asubuhi kwenda Morocco kesho.
Wachezaji wa Azam Uwanja wa Ndege wa Dubai usiku huu |
Azam inakwenda huko, ikiwa inakabiliwa na jukumu la kutoa sare ya mabao au kushinda ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Japokuwa hilo linachukuliwa kama jambo gumu mbele ya wengi, lakini rekodi ya timu hiyo, mali ya bilionea Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inaonyesha linawezekana.
Azam imekuwa ikicheza vizuri na kupata matokeo mazuri katika mechi za ugenini kwenye michuano hii, kuliko nyumbani na hata kufuzu kwake hadi hatua hii zaidi kulitokana na matokeo ya mechi za ugenini.
Raundi ya kwanza, Azam ilianza kwa kushinda kwa taabu 3-1 Dar es Salaam dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini, sehemu kubwa ya mchezo huo matokeo yakiwa 1-1 kabla ya mabao ya dakika za jioni ya Kipre Tchetche kutengeneza ushindi huo.
Mchezo wa marudiano, Azam ilishinda 5-0 ugenini na kufanya ushindi wa jumla wa 8-1, ikisonga mbele kibabe.
Raundi ya Pili, ilianza kwa ushindi wa 2-1 ugenini, Liberia dhidi ya wenyeji, Barack Young Controllers II, lakini katika mchezo wa marudiano ilibanwa kwa sare ya 0-0.
Kocha Muingereza Stewart Hall hakuipa umuhimu mechi ya Ligi Kuu Ijumaa dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga iliyoisha kwa sare ya 1-1 akiwapumzisha wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi na FAR Rabat.
Wakati mabeki Waziri Salum, Joackins Atudo, viungo Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Balou na mshambuliaji Kipre Tchetche hawakukanyaga kabisa nyasi za Uwanja wa Mkwakwani Ijumaa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alicheza kwa dakika 15 tu za mwisho- ili kuhakikisha wanakuwa vizuri Jumapili mjini Rabat.
Kutoka kikosi cha kwanza cha sasa cha Azam waliocheza dakika zote juzi ni kipa Mwadini Ally, kiungo aliyehamishiwa beki ya kulia, Himid Mao, beki David Mwantika, kiungo Humphrey Mieno na washambuliaji Brian Umony na John Bocco ‘Adebayor’.
Azam, itakuwa Rabat kwa wiki nzima hadi Jumapili itakapocheza mechi na imejipanga vema kuhakikisha inavuka hatua hii.