Kocha Stewart Hall, akiwaongoza wachezaji wake mazoezini jioni ya leo viwanja vya Maamora |
Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
AZAM FC leo imefanya mazoezi yake ya kwanza tangu iwasili nchini Morocco jana kwa ajili ya mchezo wa marudiano, Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya wenyeji AS FAR ya Rabat Jumamosi mjini hapa.
Kikosi cha Azam, kimefanya mazoezi ya saa mbili kuanzia saa 9:00 Alasiri kwa saa za hapa sawa na saa 11:00 jioni kwa saa za Dar es Salaam kwenye viwanja vya michezo vya Maamora.
Wachezaji walionekana wachangamfu na kufurahia Uwanja wa nyasi halisi waliofanyia mazoezi, katika kituo hicho chenye viwanja zaidi ya vitano vizuri, vikiwemo vyenye nyasi bandia.
Baada ya mazoezi, Kocha Muingereza, Stewart Hall alisema amefurahia mazingira ya Uwanja na ukarimu wa wenyeji kwa ujumla.
“Sina malalamiko, mazingira mazuri kila kitu safi. Mambo yanakwenda vizuri, nafurahi,”alisema Stewart.
Salum Abubakar 'Sure Boy' akimtoka Kali Ongala mazoezini |
Seif Abdallah akimtoka Humphrey Mieno. Kulia ni Waziri Salum |
Kali Ongala akiwatoka Sure Boy na Brian Umony |
Kipre Tchetche akimtoka Malika Ndeule |
John Bocco 'Adebayor' akitafuta mbinu za kumtoka Omar Mtaki. Kulia Uhuru Suleiman |
Uwanja safi, mazoezi yananoga |
Kwenye baridi watu hawachoki |
Rabat ilishinda 1-0, bao pekee la El Mahdi Naghmi dakika ya 90 kwa tik tak, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Fez.
Ushindi huo, umewafanya wazidi kuikaribia Raja Casablanca kileleni, kwa kufikisha pointi 53, baada ya kucheza mechi 25, ikizidiwa tatu na vinara hao wa ligi hiyo, waliocheza mechi moja zaidi dhidi yao katika ligi ya timu 16.
Akiwa uwanjani hapo, Stewart aliwatazama kwa makini wapinzani wake, ambao hawakucheza soka ya kuvutia sana kulinganisha na wapinzani wao, Fez huku akionekana kuandika kwenye kitabu chake mambo fulani kwa ajili ya kuyatumia kuwaelekeza wachezaji wake kuelekea mchezo huo.
Stewart akimuonyesha kitu uwanjani Kali |
Stewart akiandika kwenye kitabu chake |
Mashabiki wa Rabat |
Hicham El Fathi wa Rabat akimzuia mchezaji wa Widad Fez |
Stewart kwa makini zadi, huku akikuna kichwa...na Kali kama unavyomuona |
Baada ya mechi hiyo, Stewart alisema; “Nimewaona, kwa kweli bado sioni kama ni timu ya kutisha kwetu. Sisi ni bora kuliko wao na nina matumaini ya kufanya vizuri dhidi yao,”.
Wakati wa mchezo, japokuwa hawakuwapo watu wengi uwanjani, lakini FAR Rabat ilionekana kushangiliwa zaidi. Mashabiki wake wanajua kuhamasisha, wakiimba nyimbo nzuri na kushangilia muda wote.
Lakini pia, wanaonekana ni watu wa vurugu timu yao inapofanya vibaya. BIN ZUBEIRY ilizungumza na baadhi ya mashabiki wa Rabat, wakasema baadhi ya mashabiki wao, zaidi ya 500 wanatafutwa na Polisi baada ya kufanya vurugu wiki iliyopita walipokwenda kucheza mechi Casabalanca na ndiyo sababu leo hawakuwa wengi uwanjani.
“Wanaogopa wakionekana tu, watakamatwa na Polisi, ndiyo maana si wengi leo, ila huwa wanajaa pote pale,”alisema shabiki mmoja akionyesha eneo wanaloketi mashabiki hao, upande wa ubao wa kuonyesha matokeo.
Azam itaendelea na mazoezi kesho na Stewart amesema watafanya awamu mbili, asubuhi na jioni.
Viongozi; Kutoka kulia Jemadari, Nassor na Kahemele |
Mweusi anavutia; Bin Zubeiry akiwa katikati ya mashabiki wa Rabat na bendera yao |
Raha ya bao; Mashabiki wa Rabat wakishangilia bao la dakika ya mwisho |
Wanaondoka; Kutoka kulia Bin Zubeiry, Kahemele na Nassor |
Azam iliwasili hapa jana baada ya safari ndefu ya takriban saa 14 angani na saa mbili na ushei barabarani- saa tano kutoka Dar es Salaam hadi Dubai na saa tisa kutoka Dubai hadi Cassablanca- kisha saa mbili kwa barabara hadi Rabat.
Iliondoka Dar es Salaam Jumapili saa 11:00 jioni na kufika Dubai saa 6:00 ambako ililala hadi asubuhi ya jana ilipoondoka kuja Morocco na wachezaji walifika wamechoka kwa uchovu wa safari ndefu.
Ikumbukwe, Azam inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Afrika, inahitaji sare yoyote ya mabao au kushinda, ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa Dar es Salaa kulazimishwa sare ya bila kufungana.
Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja huo huo wa Prince Moulay Abdallah hapa Rabat, wenye uwezo wa kukusanya mashabiki 52,000 kuanzia saa 11:00 kwa saa za hapa, sawa na saa 1:00 kwa saa za nyumbani, Tanzania.