KLABU ya Arsenal imerejea katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fulham kwenye Uwanja wa Craven Cottage katika mchezo ambao kila timu ilipoteza mchezaji mmoja kwa kadi nyekundu.
Fulham wanaweza kujihesabu hawakuwa na bahati kwa kushindwa japo kuondoka na pointi moja kwenye mechi hiyo baada ya kutolewa mapema kwa kiungo Steve Sidwell - ambaye alikuwa anarejea uwanjani baada ya kumaliza adhabu ya mechi tatu kwa kumchezea rafu Mikel Arteta dakika ya 12.
Arsenal ilitumia mwanya huo kujipatia bao pekee la ushindi dakika ya 43 lililotiwa kimiani na beki Per Mertesacker kwa kichwa kabla ya Olivier Giroud kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 90 kwa kumchezea rafu Stanislav Manolev.
Katika mchezo huo, kikosi cha Arsenal kilikuwa: Szczesny, Sagna, Mertesacker, Koscielny, Monreal, Rosicky/Podolski dk71, Arteta, Ramsey, Walcott/Wilshere dk71, Giroud na Cazorla/Vermaelen dk90.
Fulham: Schwarzer, Manolev, Senderos, Hangeland, Richardson, Emanuelson/Frei dk87, Sidwell, Enoh, Kacaniklic/Petric dk85, Ruiz na Berbatov.
Chukua gwala: Per Mertesacker (kushoto) akishangilia bao lake pekee la ushindi na Nacho Monreal
Kitu nyavuni: Beki wa Arsenal, Per Mertesacker akiteleza kufunga kwa kichwa