KIUNGO chipukizi Mtanzania, Adam Nditi jana aliendelea kuwa nje wakati timu yake, Chelsea ilipolala 1-0 mbele ya Norwich ugenini, bao pekee la Cameron McGeehan dakika ya mwisho kwa penalti katika Fainali ya kwanza ya Kombe la FA la Vijana.
Mechi ilionekana itaisha kwa sare hadi beki wa Chelsea, Alex Davey alipodaiwa na refa Neil Swarbrick kumuangusha kwenye eneo la hatari Joshua Murphy katika dakika ya pili ya dakika za nyongeza.
McGeehan hakuiangusha beji yake ya Unahodha na akaenda kuukiwamisha nyavuni mkwaju wa penalti akimtungua kipa Mitchell Beeney na kuwainia kwa shangwe mashabiki wa nyumbani, Uwanja wa Carrow Road ambao walikuwa zaidi ya 22,000.
Chelsea ilitawala mchezo huo na kutengeneza nafasi nzuri, ambazo walishindwa kuzitumia, lakini waapewa nafasi kubwa ya kuupiku ushindi huo mwembamba katika mchezo wa marudiano nyumbani, Uwanja wa Stamford Bridge wiki ijayo.
Sasa ni mwezi wa pili, Nditi anayetokea visiwani Zanzibar anakosekana kabisa katika kikosi cha Chelsea, hata benchi hakai na haijulikani nini kinachomsibu kama ni majeruhi au amepokonywa namba.
Lakini BIN ZUBEIRY itaendelea kufuatilia ili kujua ukweli juu ya kiungo huyo aliyebeba matumaini ya Watanzania wengi kwamba ataling'arisha jina la nchi yake katika klabu kubwa Ulaya.
Kikosi cha Norwich City kilikuwa: Britt, Norman, Wyatt, McGeehan, McFadden, Toffolo, Murphy, Randall, Morris, King/Young na Murphy.
Chelsea: Beeney, Aina, Davey, Ake, Wright, Baker, Kiwomya, Loftus-Cheek, Feruz/Musonda, Colkett/Swift na Boga.
La ushindi jioni: Nahodha wa Norwich, Cameron McGeehan akifunga kwa penalti. Chini anapongezwa na wenzake.