![]() |
Abbel Dhaira akiwa amedaka moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake jana |
Na Suleiman Shineni
KIPA Mganda wa Simba SC, Abbel Dhaira jana alijaribiwa zaidi kuliko kipa wa Azam FC, Mzenji Mwadini Ally wakati timu zao zilipomenyana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao timu hizo zilifungana mabao 2-2, bado Dhaira pia alionekana kufungwa mabao yasiyo rahisi, tofauti na Mwadini.
Mwadini alifungwa kwa aina moja mabao yote, kwanza akiruhusu krosi kupita hadi upande wa pili kutoka kwa mtu yule yule, Mrisho Ngassa na kumkuta mtu yule yule, Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyefunga mara mbili.
Lakini Dhaira alifungwa bao la kwanza kwa penalti na Kipre Tchetche baada ya Khamis Mcha ‘Vialli’ kuangushwa kwenye eneo la hatari na William Lucian ‘Gallas’.
Bao la pili, mpira wa adhabu wa Mcha uliunganishwa nyavuni na Humphrey Mieno, lakini Dhaira alionekana kusita kuucheza baada ya mfungaji kuonekana ameupiga kwa mkono, ingawa refa Orden Mbaga alihalalisha bao hilo.
Kwa ujumla katika mchezo wa jana, Dhaira alidaka mipira saba, tena ile kuificha kabisa, wakati mitatu aliipangua- ina maana alipigiwa mipira 10 iliyolenga lango lake.
Kwa Mwadini, pamoja na kufungwa mabao mawili, lakini alionyesha pia ni kipa imara baada ya kudaka mipira nane.
Dhaira jana alidaka mechi ya sita tangu ajiunge na Simba SC Januari mwaka huu na kufungwa jumla ya mabao 11 katika mechi hizo. Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Bandari katika Kombe la Mapinduzi, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 akifungwa bao moja kwa penalti.
Alidaka pia Simba ikimenyana na U23 ya Oman, akafungwa moja, timu yake ikilala 1-0, akadaka dhidi ya Al Qaboos Simba ikilala 3-1, yeye akitokea benchi na kufungwa mawili, lingine Juma Kaseja aliyeanza.
Akadaka tena dhidi ya Recreativo do Libolo nchini Angola, akafungwa mabao manne Simba ikilala 4-0. Akadata tena dhidi ya Coastal Union Simba SC ikishinda 2-1, akifungwa bao moja kabla ya jana kutunguliwa mara mbili.
Simba SC ndio timu inayoonekana kuwa na walinda milango bora nchini, wote wakiwa makipa wa kwanza wa timu zao za taifa, Juma Kaseja kwa Tanzania na Dhaira kwa Uganda.